• HABARI MPYA

    Sunday, July 14, 2013

    MICHO AWASHANGAA YANGA SC KUHUSU KIIZA

    Na Mahmoud Zubeiry, IMEWEKWA JULAI 14, 2013 SAA 3:00 ASUBUHI
    KOCHA Mkuu wa Uganda, Mserbia Milutin Sredojevich ‘Micho’ amewashangaa mno Yanga SC hadi sasa kuwa hawajasaini Mkataba na mshambuliaji Hamisi Friday Kiiza ‘Diego’, kwani mchezaji huyo kwa sasa ni lulu.
    “Yanga wasimdharau Kiiza hata kidogo, yule ni tegemeo la Uganda na anaweza kwenda Ulaya wakati wowote. Kiiza ndiye aliyeiwezesha Uganda kuifunga Angola (mechi ya kuwania tiketi ya Kombe la Dunia mwezi uliopita). Wanatakiwa kumsaini kwa ofa nzuri, ili awatumikie vizuri,”alisema Micho akizungumza na BIN ZUBEIRY jana.
    Micho alimwagia sana sifa Kiiza jana akisema kwamba ni mchezaji anayejituma na jasiri, ambaye katika mchezo na Angola alikuwa akiwavaa mabeki wenye miilii mikubwa hadi akaipatia Uganda penalti na kumponza mchezaji wa wapinzani wao hao kutolewa nje kwa kadi nyekundu.
    Kiiza, au ‘Diego wa Kampala’ alitua Alasiri ya jana mjini Dar es Salaam kwa ndege ya Shirika la Kenya (KQ) tayari kusaini Mkataba wa kuendelea kuitumikia Yanga SC kwa miaka mingine miwili. 
    Kiiza akiwa na Seif Magari Taifa jana

    Hiyo inafuatia mpachika mabao huyo kufikia makubaliano na Yanga juu ya dau la usajili, baada ya awali kushindana hadi akarejea kwao, Kampala na ikaripotiwa alikuwa karibuni kusaini URA ya kwao.
    Mfanyabiashara mwenye jina mjini, Mussa Katabaro alikwea pipa hadi Uganda wiki mbili zilizopita kufanya mazungumzo ya kina na Kiiza ili abaki Yanga na hatimaye akakubali kuendelea kuvaa jezi za kijani na njano kwa miaka mingine miwili.
    Kiiza alikuwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam jana wakati Tanzania inafungwa 1-0 na Uganda akiwa ameketi na vigogo wa usajili wa klabu hiyo, Seif Ahmad ‘Magari’, Abdallah Ahmad ‘Bin Kleb’ na Mussa Katabaro.
    Katabaro ambaye ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga SC na mmoja wa Wajumbe wa Kamati ya Mashindano, chini ya Mwenyekiti Abdallah Bin Kleb ameiambia BIN ZUBEIRY jana kwamba Kiiza atasaini Yanga SC leo.
    Katabaro alipokuwa Kampala katika mazungumzo yake na Diego walikubaliana kumuongezea Mkataba wa miaka miwili kwa dau la dola za Kimarekani 40,000 na mshahara wa dola 1,500 kwa mwezi.
    Lakini Katabaro akaomba Kiiza akubali kuchukua dola 20,000 kwa sasa na dola 20,000 nyingine atampa katika mwanzo wa mwaka wa pili wa Mkataba wake. Kiiza akasema anataka dola 40,000 kamili kwa sababu ana kitu anataka kufanya na ndiyo maana alikataa kupokea dola 35,000 na gari, ili pate fedha kamili.
    URA  ilikuwa tayari kumsaini Kiiza kwa mshahara wa dola 1,000 na dau la usajili dola 40,000 kama ambazo ameahidiwa Jangwani.
    Awali, Kiiza aligoma kusaini Yanga kutokana na kulazimishwa achukue dola 35,000 na dola 5,000 nyingine apewe gari.
    Kiiza anaishi Uganda na Tanzania yupo kwa ajili ya kazi na haoni umuhimu wa kumiliki gari Dar es Salaam, hivyo anataka fedha, lakini Yanga watu wanaohusika na usajili Yanga iliadaiwa walikuwa wanamlazimisha achukue na gari.
    Kiiza alimaliza vizuri Mkataba wake wa kwanza wa miaka miwili Yanga SC kwa kufunga bao zuri la ushindi dhidi ya mahasimu, Simba SC miezi miwili iliyopita Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wana Jangwani wakiibuka na ushindi wa 2-0, bao la kwanza likifungwa na Mrundi, Didier Kavumbangu.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: MICHO AWASHANGAA YANGA SC KUHUSU KIIZA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top