Na Oscar Asenga, Tanga, IMEWEKWA AGOSTI 7, 2013 SAA 2:53 USIKU
MAPOKEZI wa Mshambuliaji Mpya wa Klabu ya Coastal Union ya Tanga aliyetokea timu ya Mamlaka ya Mapato nchini Uganda (URA),Yayo Lutimba kwenye uwanja wa Ndege Mkoani Tanga jana yalikuwa ya aina yake kutokana na kulakiwa na wingi wa mashabiki,viongozi na wanachama wa timu hiyo.
Mapokezi hayo yalianza saa mbili asubuhi na mchezaji huyo kutua saa nne katika uwanja wa ndege akiwa na Meneja wa timu hiyo Akida Machai ambaye alikuwa ameambatana naye kutoka nchini Uganda.
Mshambuliaji wa Mpya wa klabu ya Coastal Union ya Tanga Yayo Lutimba akitoka uwanja wa Ndege wa Tanga mara baada ya kutua akitokea nchini Uganda kushoto kwake ni Meneja wa timu ya Coastal Union Akida Machai ambaye alimfuata nchini humo.
Awali aliripotiwa katika gazeti la Uganda New Vision la jana (juzi) liliripoti kuwa mchezaji huyo alisajiliwa na Yanga ya Tanzania.
Akizungumza katika mapokezi hayo,Katibu wa Klabu ya Coastal Union ya Tanga,Kassim Eli Siagi alisema wameingia mkataba wa miaka miwili na mchezaji huyo ambaye ataitumia timu hiyo kuanza msimu mpya wa ligi kuu utakaoanza Agosti 24 mwaka huu.
El Siagi alisema kuwepo kwa mchezaji huyo katika kikosi kuteleta chachu na upinzani mkubwa na hivyo kuipa mafanikio timu hiyo.
Katibu Mkuu wa Klabu ya Coastal Union ya Tanga, Kassim El Siagi kulia mwenye shati la mistari meupe katikati ni Mshambuliaji huyo Yayo Lutimba na kulia ni shabiki wa timu hiyo Miraji Wandi.
Awali akizungumza mara baada ya kuwasili uwanjani hapo,Lutimba alihaidia kucheza kwa kujituma ili kuweza kuipa mafanikio timu hiyo pamoja na kushirikiana na wachezaji wenzake ili kutimiza malengo yao.