• HABARI MPYA

    Sunday, September 08, 2013

    STARS ILISTAHILI KUFUNGWA NA GAMBIA, ASEMA KOCHA KIM

    Na Boniface Wambura, IMEWEKWA SEPTEMBA 8, 2013 SAA 6:48 USIKU
    KOCHA Mkuu wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Mdenmark Kim Poulsen amesema timu yake ilistahili kufungwa na Gambia jana katika mchezo wa mwisho wa Kundi C kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Dunia kwa kuwa wapinzani walitengeneza nafasi nyingi kuliko timu yake.
    Pamoja na hayo, Kim amesema kwamba Gambia walipata mabao mepesi jana katika mchezo huo uliofanyika kwenye Uwanja wa Independence, Banjul.
    Furaha imetoweka; Kocha wa Stars Kim Poulsen amesema timu ilistahili kipigo cha Gambia

    “Hatukutengeneza nafasi nyingi za kufunga, lakini tukaruhusu mabao mapesi. Nawapongeza Gambia kwani walistahili ushindi. Unapofanya makosa unaadhibiwa. Gambia ilikuwa timu nzuri leo, kwani ilitengeneza nafasi nyingi za kufunga, sisi tukatoa mabao mepesi,” amesema Kim. 
    Hata hivyo, Kim amesema sababu nyingine ya kutofanya vizuri ni kuwakosa wachezaji wanaocheza nje ya nchi na wengine wa kikosi cha kwanza ambao ni majeruhi.
    Wenyeji Gambia walishinda 2-0, huo ukiwa ni ushindi wao wa kwanza katika kundi hilo la C ambapo imemaliza ikiwa ya mwisho ikiwa na pointi nne.
    Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager imemaliza katika nafasi ya tatu katika kundi hilo lililokuwa na timu nne ikiwa na pointi sita ilizozipata nyumbani kwa kuzifunga Morocco na Gambia.
    Mabao yote ya Gambia katika mechi hiyo iliyochezeshwa na Munyemana Hudu kutoka Rwanda yalifungwa na nahodha wa timu hiyo Mustapha Jaju dakika ya 44 na 51, na yote yaliyotokana na wachezaji wa Stars kutokuwa makini.
    Taifa Stars inaondoka Banjul leo (Septemba 8 mwaka huu) saa 6 mchana kwa ndege ya Arik hadi Dakar, Senegal ambapo itaunganisha kwa ndege ya Kenya Airways kupitia Nairobi ambapo itawasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) kesho (Septemba 9 mwaka huu) saa 8.05 mchana.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: STARS ILISTAHILI KUFUNGWA NA GAMBIA, ASEMA KOCHA KIM Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top