• HABARI MPYA

    Friday, September 13, 2013

    YANGA YAPEWA SIKU 14 KUWALIPA AKINA NSAJIGWA

    Na Boniface Wambura, IMEWEKWA SEPTEMBA 13, 2013 SAA 8:47 MCHANA
    KLABU ya Yanga imepewa siku 14 kuanzia leo (Septemba 13 mwaka huu) kuwalipa waliokuwa wachezaji wake msimu uliopita, nahodha Shadrack Nsajigwa na Stephen Mwasika wanaoidai klabu hiyo jumla ya sh. milioni 15.5.
    Uamuzi huo umefanywa na Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) iliyokutana jana (Septemba 12 mwaka huu) ambapo pamoja na mambo mengine ilisikiliza madai ya wachezaji hao.
    Nsajigwa Shadrack

    Fedha hizo ni ada ya usajili ambayo klabu hiyo ilikubaliana na wachezaji hao wakati ikiwasainisha mikataba. Yanga imeshawalipa sehemu ya fedha walizokubaliana na kiasi hicho ndicho bado hakijalipwa. Nsajigwa anadai sh. milioni 9 wakati Mwasika ni sh. milioni 6.5.
    Wakati huo huo: Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) inaingia raundi ya tatu kesho (Septemba 14 mwaka huu) kwa timu zote 14 kushuka viwanjani huku masikio ya washabiki wengi yakielekezwa kwenye mechi kati ya Simba na Mtibwa Sugar na ile kati ya Mbeya City na Yanga.
    Simba inaikaribisha Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mechi itakayochezeshwa na mwamuzi Dominic Nyamisana kutoka Dodoma. Viingilio katika mechi hiyo vitakuwa sh. 5,000 viti vya bluu na kijani, sh. 8,000 viti vya rangi ya chungwa, sh. 15,000 VIP C na B wakati VIP A itakuwa sh. 20,000.
    Pia Azam TV itautumia mchezo huo kwa ajili ya mazoezi (broadcast training) kwa wafanyakazi wake. Hivyo mechi hiyo haitarekodiwa au kuoneshwa moja kwa moja.
    Katika Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya, shughuli itakuwa kati ya mabingwa watetezi Yanga na wenyeji wao Mbeya City SC. Mwamuzi Andrew Shamba kutoka Pwani ndiye atakayepuliza filimbi wakati Kamishna wa mechi hiyo James Mhagama kutoka Songea.
    Mechi nyingine za ligi hiyo ni Coastal Union na Tanzania Prisons (Uwanja wa Mkwakwani, Tanga), Ruvu Shooting na Mgambo Shooting (Uwanja wa Mabatini mkoani Pwani), Oljoro JKT na Rhino Rangers (Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Kaluta Amri Abeid, Arusha), Kagera Sugar na Azam (Uwanja wa Kaitba, Bukoba), na Ashanti United na JKT Ruvu (Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam).
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: YANGA YAPEWA SIKU 14 KUWALIPA AKINA NSAJIGWA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top