• HABARI MPYA

    Tuesday, January 07, 2014

    CAF YAMPA LESENI YA HADHI YA JUU KOCHA ALIYETIMULWA SIMBA SC

    Na Boniface Wambura, Ilala
    ALIYEKUWA kocha Msaidizi wa klabu ya Simba ya Dar es Salaam, Jamhuri Mussa Kihwelo ‘Julio’ ametunukiwa leseni ya daraja B ya ufundishaji kandanda na Shirikisho la Soka Afrika (CAF), baada ya kuhitimu vizuri mafunzo yaliyofanyika mwaka jana visiwani Zanzibar.
    Julio aliyekuwa Msaidizi wa mchezaji mwenzake wa zamani wa Simba SC, Alhaj Abdallah Athumani Seif ‘King Kibadeni’  walifukuzwa baada ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu msimu na nafasi zao kuchukuliwa na Mcroatia Zdravko Logarusic na mzalendo Suleiman Matola ‘Veron’.
    Julio kulia akiwa na King Kibadeni enzi zao Simba SC 

    Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Mwesigwa Selestine leo amemkabidhi Julio leseni yake pamoja na za makocha wote wengine walioshiriki kozi iliyofanyika mjini Zanzibar mwaka jana ambao hawakuwepo.
    Makocha wengine waliofuzu kozi hiyo iliyoendeshwa na mkufunzi Bhekisisa Boy Mkhonta kutoka Swaziland ni Abdulghan Msoma, Hafidh Badru, Nasra Juma Mohamed, Gulam Abdallah Rashid, Mohamed Ayoub Suleiman, Shaaban Ramadhan, John Simkoko na Hemed Suleiman Ali. Hivi sasa Tanzania ina makocha 40 wenye leseni B za CAF baada ya wengine 31 kufuzu katika mafunzo yaliyofanyika mapema mwaka juzi jijini Dar es Salaam chini ya mkufunzi Honor Janza kutoka Zambia.
    Katika hatua nyingine, waamuzi na makamisaa wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) na Ligi Daraja la Kwanza (FDL) watashiriki semina itakayofanyika Januari 13 na 14 mwaka huu jijini Dar es Salaam, ambayo itafunguliwa na Rais wa TFF, Jamal Malinzi.
    Wakati huo huo, Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) kimemwalika Rais Malinzi kuwa mgeni rasmi kwenye mechi ya robo fainali ya Kombe la Mapinduzi kati ya Simba na Chuoni itakayochezwa kesho kuanzia Saa 2:00 usiku Uwanja wa Amaan.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: CAF YAMPA LESENI YA HADHI YA JUU KOCHA ALIYETIMULWA SIMBA SC Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top