• HABARI MPYA

    Friday, January 10, 2014

    NASSOR MOHAMMED: OZIL WA ZENJI ALIYETUA NA KUPEPERUKA MSIMBAZI

    Na Mahmoud Zubeiry, Zanzibar
    APRILI mwaka jana kikosi cha pili cha Simba, maarufu kama Simba B kilipokea mchezaji mpya kutoka visiwani Zanzibar na wakati anaanza kupigiwa hesabu kubwa na klabu hiyo, ndani ya mwezi mmoja akaondoka katika timu hiyo.
    Huyo ni Nassor Mohammed Nassor, ambaye amepewa jina la utani, Ozil akifananishwa na kiungo wa kimataifa wa Ujerumani na klabu ya Arsenal ya England, Mesut Ozil, si kwa sura bali uchezaji mzuri katika nafasi ya kiungo.
    Ozil wa Zenji; Nassor Mohammed alitua Simba B, lakini akaondoka baada ya kupata nafasi Oman

    “Nilipofika Simba B, nilikubalika na wakasema nikiendelea vizuri, dirisha dogo na mimi nitapandishwa kikosi cha kwanza kama akina Messi (Ramadhani Singano), lakini kwa bahati nzuri, nikapata nafasi ya majaribio nje ya nchi, ikabidi niondoke Simba B,”anasema Nassor katika mahojiano na BIN ZUBEIRY visiwani hapa jana.  
    Nassor anasema kwamba alikwenda Oman Juni mwaka jana kufanya majaribio klabu ya Al Hamra ya Daraja la pili nchini humo na akafanikiwa kufuzu licha ya ushindani kutoka kwa wachezaji wengine waliokuwa wakiwania nafasi.
    “Tulikuwa wachezaji watatu na anatakiwa mmoja, mmoja alikuwa anatokea Nigeria na mwingine Mali, lakini mimi ndiyo nikakubalika na kuambiwa nibaki, wale wengine wakaondoka. Lakini sijui kikatokea nini, baadaye klabu ikasema haiwezi kuchukua mchezaji wa kigeni tena,”.
    Nassor alianza kushinda mataji tangu akiwa kinda na timu yake ya mtaani, Arizona
    Nassor akifanya mazoezi Oman
    Nassor akiwa katika nyumba aliyopewa Oman

    “Mimi nikalazimika kuondoka na mwezi Oktoba mwaka jana nikarudi nchini, ila kwa bahati mbaya usajili huku ulikuwa umekwishafungwa. Nikaamua kujiunga na Malindi kufanya nao mazoezi, wakanikubali na sasa wananisajili katika dirisha dogo nicheze ligi mwaka huu,”anasema. 
    Kwa nini hakurudi Simba B? “Unajua nilipopata nafasi ya Oman, sikuaga Simba, niliondoka tu, sasa nilipokwama nikaona aibu kurudi kule, ila hata hapa Malindi si pabaya, naamini nikifanya vizuri hao Simba, Yanga na Azam watanisajili tu,”anasema.  
    Kutokana na soka yake nzuri, tayari Nassor amefanikiwa kuingia Mkataba na wakala wa wachezaji anayetambuliwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), Said Maaskary ambaye anafanya shughuli zake Oman na nchi nyingine za Asia.
    Nassor alipokuwa Oman

    “Mimi nina mkataba na wakala mmoja anaitwa Said Maaskary, ambaye ndiye alinipatia nafasi ya Oman, kwa hivyo naamini tu nikijitahidi kufanya vizuri, nitatimiza ndoto zangu za kucheza nje muda si mrefu.
    Nassor Mohamed Nassor alizaliwa Aprili 22, mwaka 1994, eneo la Mfenesini, Zanzibar na alipata elimu yake ya Msingi katika shule ya Mfenesini na baadaye sekondari ya Lumumba visiwani humo hadi kidato cha sita.
    Soka ‘Ozil wa Zenji’ alianza kucheza tangu akiwa shule ya msingi na mara kadhaa aliitwa katika vikosi vya kombaini za Copa Coca Cola na Airtel Rising Stars vya Mjini Magharibi, lakini akashindwa kwenda kwa sababu wazazi wake walitaka asome.
    Wakati akisoma na kucheza shuleni, lakini pia Nassor alikuwa akichezea timu ya mtaani kwao, Arizona ya Malindi ambayo ilikuwa ya vijana, kabla ya mwaka 2009 kusajiliwa na klabu ya Daraja la Pili, Machimbo FC.
    Katika jitihada za kusaka mafanikio kwenye soka, alipomaliza Kidato cha Sita mwaka jana, akaenda Simba B, ambako baada ya muda mfupi alipata nafasi ya majaribio Oman. 
    Sasa Nassor anatarajiwa kuichezea Malindi katika Ligi kuanzia mwezi ujao, ili kukipambanua zaidi kipaji chake na anasema ndoto zake ni kucheza Ulaya siku moja. Huyo ndiye Ozil wa Zenji, Nassor Mohamed Nassor, kinda wa visiwani Zanzibar aliyetua na kupeperuka Simba B.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: NASSOR MOHAMMED: OZIL WA ZENJI ALIYETUA NA KUPEPERUKA MSIMBAZI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top