• HABARI MPYA

    Wednesday, October 10, 2012

    AZIM DEWJI AMFICHUA MBAYA WA YANGA

    Azim Dewji

    Na Princess Asia
    MFANYABIASHARA maarufu nchini na mfadhili wa zamani wa Simba, Azim Dewji amesema baadhi ya wanahabari nchini wanachangia matokeo mabaya ya Yanga katika michuano ya mwaka huu ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
    Amesema wamekuwa wakiingiza zaidi ushabiki, badala ya kuisaidia timu hivyo kuwafanya wachezaji kulewa sifa mapema hata pasipostahili, hali inayozifanya klabu nyingine kucheza kwa kukamia kwa hofu ya kubebesha kapu la magoli.
    Dewji aliyasema hayo jana, alipokuwa anazungumzia kupepesuka kwa Yanga, licha ya kufanya usajili tishio msimu huu.
    Katika mechi sita za ligi msimu huu, Yanga imeshapoteza mechi mbili, imetoka sare mara mbili na kushinda mara mbili, hivyo kuifanya kufikisha pointi nane ambazo ni nusu ya pointi zilizokusanywa na watani wao Simba wanaoongoza ligi baada ya kukusanya pointi 16 kutokana na mechi sita pia.
    Akiichambua Yanga, alisema imesajili vizuri, lakini waandishi wa habari wamechangia kuwavimbisha vichwa wachezaji kwa kuupamba mno usajili wao, ilhali ni wachezaji wa kawaida.
    “Kama mwanamichezo, sioni tatizo kwa timu wala benchi la ufundi, nadhani waandishi wanaoishabikia Yanga wanaimaliza timu yao bila kujijua. Wanaikuza mno kuanzia kipindi cha usajili..kila anayesajiliwa anapambwa kupita maelezo.
    “Matokeo yao wanavimba vichwa, mashabiki wanajazwa matumaini makubwa, na timu pinzani, hata kama ni ndogo zinakamia zikihofia kugeuzwa kapu la magoli na hii timu inayotajwa kuwa tishio kabisa, wakati ukweli sivyo…” anasema.
    Aliongeza kusema: “Nashukuru Simba tulifungwa na Azam 3-1 katika Kagame. Ile ilitushitua, tukatuliza akili na ndiyo maana unaona timu imesukwa upya na iko imara. Tungetwaa ubingwa hakika Simba hii ingekuwa nyeupe, tungelewa sifa tu. Soka haiko hivyo, kwa hiyo waandishi wasiegemee ushabiki pekee, wazisaidie timu zao pia.”
    Dewji alisisitiza kuwa, pamoja na nia ya kufanya biashara, vyombo vya habari vinapaswa kusimama katika ukweli, badala ya kusifia kila kinachoonekana, huku mambo yasiyofaa yakifunikwa kwa hofu ya kuwakera wahusika.
    “Haya yanayotokea katika soka, hasa Simba na Yanga hayana tofauti na jinsi waandishi wanavyojaribu kukuza kila kitu cha Chadema, kiasi cha kujiona wamefika juu mno kisiasa, sikatai ni chama chenye wafuasi wengi, lakini washauriwe jinsi ya kujipanga hatua kwa hatua kuliko
    kuwajaza matumaini na matokeo yake utakuta kila kinachofanyika, wanajiona wanaonewa…waandishi wawe washauri wazuri jamani,” alisema Dewji.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: AZIM DEWJI AMFICHUA MBAYA WA YANGA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top