• HABARI MPYA

    Wednesday, October 10, 2012

    NGASSA, KIGGI WAENGULIWA SAFARI YA SIMBA TANGA GHAFLA

    Ngassa

    Na Prince Akbar
    VIUNGO wa zamani wa Yanga, Mrisho Khalfan Ngassa na Kiggi Makassy Kiggi wameenguliwa katika kikosi cha Simba kilichoondoka leo kwenda Tanga kwa ajili ya mchezo wa Jumamosi wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, dhidi ya wenyeji Coastal Union kwenye Uwanja wa Mkwakwani.
    Ofisa Habari wa Simba SC, Ezekiel Kamwaga amesema kwamba, Ngassa ameondolewa kwa sababu bado hajapona Malaria iliyomkosesha mechi iliyopita ya ligi hiyo dhidi ya JKT Oljoro ya Arusha, wakati Makassy aliumia jana kwenye mchezo wa kirafiki dhidi ya Azam FC.
    Awali, Kamwaga alisema leo mchana kwamba, katika safari hiyo timu hiyo itawakosa nyota watano, Emanuel Okwi ambaye amekwenda kujiunga na timu yake ya taifa, Uganda, Ramadhani Chombo ‘Redondo’ anayesumbuliwa na Malaria, Haruna Shamte, Hamadi Waziri na Komabil Keita ambao ni majeruhi.
    Aliwataja wachezaji 22 waliokwenda na timu Tanga ni makipa Juma Kaseja, Wilbert Mweta, mabeki Nassor Masoud ‘Chollo’, Amir Maftah, Juma Nyoso, Paschal Ochieng, Shomary Kapombe, Hassan Khatib, Paulo Ngalema, Komabil Keita, viungo Mwinyi Kazimoto, Jonas Mkude, Amri Kiemba, Salim Kinje, Ramadhani Singano, Uhuru Suleiman, Haruna Moshi ‘Boban’ na washambuliaji Felix Sunzu, Edward Christopher, Haroun Chanongo, Daniel Akuffo na Abdallah Juma.
    Katika kujiandaa na mechi ya Tanga, Simba jana ilicheza mechi ya kujipima nguvu na kuifunga Azam FC mabao 3-2 katika mchezo wa kirafiki uliofanyika asubuhi kwenye Uwanja wa Chamazi, maarufu kama Azam Complex, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
    Mabao ya Simba leo yalifungwa Ramadhani Singano ‘Messi’, Uhuru Suleiman ‘Robinho’ na Daniel Akuffo, wakati ya Azam yalifungwa na Jamil Mchauru na Khamis Mcha.
    Hiyo ilikuwa mechi ya nne Azam inafungwa na Simba msimu huu katika mechi tano walizokutana hadi sasa, baada ya awali kufungwa kwa penalti kwenye fainali ya Kombe la Urafiki, kufuatia sare ya 2-2, kufungwa 2-1 kwenye Nusu Fainali ya BancABC Sup8R na 3-2 kwenye mechi ya Ngao ya Jamii, wakati wao walishinda 3-1 dhidi ya Wekundu hao wa Msimbazi, katika Robo Fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame.
    Azam na Simba zitakutana tena katika mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, mzunguko wa kwanza, Oktoba 27, mwaka huu, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.     
    Simba ndio inaongoza Ligi Kuu, hadi sasa ikiwa imeshinda mechi tano kati ya sita ilizocheza na moja tu imetoka sare, hivyo kujikusanyia pointi 16, wakati Azam inashika nafasi ya pili ikizidiwa pointi tatu, ingawa pia iko nyuma kwa mchezo mmoja.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: NGASSA, KIGGI WAENGULIWA SAFARI YA SIMBA TANGA GHAFLA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top