• HABARI MPYA

    Friday, October 12, 2012

    SIMBA SC IPO KAMILI KWA GAME LA KESHO TANGA


    Wachezaji wa Simba SC wakipasha

    Na Prince Akbar
    SIMBA inaendelea vizuri kwa maandalizi yake ya mchezo wa kesho dhidi ya wenyeji Coastal Union mjini Tanga na wachezaji wote 22 waliokwenda huko wana morali ya kutosha ya ushindi.
    Vigogo wa Friends Of Simba (F.O.S) wakiongozwa na Mwenyekiti wao, Zacharia Hans Poppe wamekodi ndege kwenda Tanga kuwaongezea morali washinde mechi ya kesho, ambayo inatarajiwa kuwa ngumu kutokana wenyeji kupania kuwa timu ya kwanza kuifunga Simba msimu huu.
    Ikumbukwe Simba imetoa sare moja ya kufungana 1-1 na Yanga, Oktoba 3, mwaka huu katika mechi zake sita ilizocheza sasa na nyingine zote tano imeshinda, jambo ambalo linawafanya waendelee kuwa kileleni mwa Ligi Kuu.
    Simba, ambayo kwenye mechi hiyo itawakosa nyota wake saba, Emanuel Okwi ambaye amekwenda kujiunga na timu yake ya taifa, Uganda, Ramadhani Chombo ‘Redondo’, Mrisho Khalfan Ngassa wanaosumbuliwa na Malaria, Haruna Shamte, Kiggi Makassy Kiggi, Hamadi Waziri na Komabil Keita ambao ni majeruhi ipo Tanga tangu juzi.
    Wachezaji 22 walio na timu Tanga ni makipa Juma Kaseja, Wilbert Mweta, mabeki Nassor Masoud ‘Chollo’, Amir Maftah, Juma Nyoso, Paschal Ochieng, Shomary Kapombe, Hassan Khatib, Paulo Ngalema, Komabil Keita, viungo Mwinyi Kazimoto, Jonas Mkude, Amri Kiemba, Salim Kinje, Ramadhani Singano, Uhuru Suleiman, Haruna Moshi ‘Boban’ na washambuliaji Felix Sunzu, Edward Christopher, Haroun Chanongo, Daniel Akuffo na Abdallah Juma.
    Katika kujiandaa na mechi ya Tanga, Simba Jumanne ilicheza mechi ya kujipima nguvu na kuifunga Azam FC mabao 3-2 katika mchezo wa kirafiki uliofanyika asubuhi kwenye Uwanja wa Chamazi, maarufu kama Azam Complex, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
    Mabao ya Simba siku hiyo yalifungwa Ramadhani Singano ‘Messi’, Uhuru Suleiman ‘Robinho’ na Daniel Akuffo, wakati ya Azam yalifungwa na Jamil Mchauru na Khamis Mcha.
    Hiyo ilikuwa mechi ya nne Azam inafungwa na Simba msimu huu katika mechi tano walizokutana hadi sasa, baada ya awali kufungwa kwa penalti kwenye fainali ya Kombe la Urafiki, kufuatia sare ya 2-2, kufungwa 2-1 kwenye Nusu Fainali ya BancABC Sup8R na 3-2 kwenye mechi ya Ngao ya Jamii, wakati wao walishinda 3-1 dhidi ya Wekundu hao wa Msimbazi, katika Robo Fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame.
    Azam na Simba zitakutana tena katika mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, mzunguko wa kwanza, Oktoba 27, mwaka huu, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.     
    Simba ndio inaongoza Ligi Kuu, hadi sasa ikiwa imeshinda mechi tano kati ya sita ilizocheza na moja tu imetoka sare, hivyo kujikusanyia pointi 16, wakati Azam inashika nafasi ya pili ikizidiwa pointi tatu, ingawa pia iko nyuma kwa mchezo mmoja.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: SIMBA SC IPO KAMILI KWA GAME LA KESHO TANGA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top