• HABARI MPYA

    Wednesday, October 10, 2012

    SIMBA WAENDA TANGA MCHANA HUU BILA NYOTA WATANOI KUIVAA COASTAL UNION

    Basi la Simba safari ya kwanza Tanga

    Na Mahmoud Zubeiry
    SIMBA SC inaondoka kwa basi lake mchana huu kwenda Tanga, tayari kwa mchezo wa Jumamosi wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, dhidi ya wenyeji Coastal Union kwenye Uwanja wa Mkwakwani.
    Ofisa Habari wa Simba SC, Ezekiel Kamwaga amewaambia Waandishi wa Habari mchana huu kwamba, katika safari hiyo timu hiyo itawakosa nyota watano, Emanuel Okwi ambaye amekwenda kujiunga na timu yake ya taifa, Uganda, Ramadhan Chombo ‘Redondo’ anayesumbuliwa na Malaria, Haruna Shamte, Hamadi Waziri na Komabil Keita ambao ni majeruhi.
    Kamwaga alisema kwamba Mrisho Ngassa aliyekuwa anaumwa Malaria amepona na yumo kwenye msafara wa mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu unaokwenda Tanga kwa basi jipya la kisasa, walilopewa na wadhamini wao, Kampuni ya Bia Tanzania (TBL).
    Katika kujiandaa na mechi ya Tanga, Simba jana ilicheza mechi ya kujipima nguvu na kuifunga Azam FC mabao 3-2 katika mchezo wa kirafiki uliofanyika asubuhi kwenye Uwanja wa Chamazi, maarufu kama Azam Complex, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
    Mabao ya Simba leo yalifungwa Ramadhani Singano ‘Messi’, Uhuru Suleiman ‘Robinho’ na Daniel Akuffo, wakati ya Azam yalifungwa na Jamil Mchauru na Khamis Mcha.
    Hiyo ilikuwa mechi ya nne Azam inafungwa na Simba msimu huu katika mechi tano walizokutana hadi sasa, baada ya awali kufungwa kwa penalti kwenye fainali ya Kombe la Urafiki, kufuatia sare ya 2-2, kufungwa 2-1 kwenye Nusu Fainali ya BancABC Sup8R na 3-2 kwenye mechi ya Ngao ya Jamii, wakati wao walishinda 3-1 dhidi ya Wekundu hao wa Msimbazi, katika Robo Fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame.
    Azam na Simba zitakutana tena katika mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, mzunguko wa kwanza, Oktoba 27, mwaka huu, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.      
    Simba ndio inaongoza Ligi Kuu, hadi sasa ikiwa imeshinda mechi tano kati ya sita ilizocheza na moja tu imetoka sare, hivyo kujikusanyia pointi 16, wakati Azam inashika nafasi ya pili ikizidiwa pointi tatu, ingawa pia iko nyuma kwa mchezo mmoja.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: SIMBA WAENDA TANGA MCHANA HUU BILA NYOTA WATANOI KUIVAA COASTAL UNION Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top