• HABARI MPYA

    Friday, October 12, 2012

    SURE BOY JR. SASA KAMILI KUIBEBA AZAM LIGI KUU

    Salum Abubakar 'Sure Boy Jr.'

    Na Mahmoud Zubeiry
    KIUNGO bora Afrika Mashariki kwa sasa, Salum Abubakar ‘Sure Boy Jr.’ amepona kabisa na ameongozana na kikosi cha klabu yake Azam FC kilichokwenda Morogoro, kwa ajili ya mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya wenyeji Polisi kesho kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.
    Sure amekuwa majeruhi kwa muda mrefu na msimu tangu uanze alijaribu kuingizwa kwenye mechi tatu, lakini akashindwa kucheza vema kutokana na maumivu, aliyoyapata kwenye michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, Julai mwaka huu.
    Aliingia akitokea benchi kwenye mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya Simba, ambayo Azam ililala 3-2 na akaingia tena kwenye mechi na JKT Ruvu ambayo Azam ilishinda 3-0 na mechi iliyopita dhidi ya African Lyon, ambayo Azam ilishinda 1-0, Sure aliingia tena akitokea benchi.
    Kama ataanza kwenye mechi ya kesho na Polisi, hiyo itakuwa ya kwanza kwake tangu kuanza kwa Ligi Kuu na kulingana na maendeleo ya afya yake, kuna uwezekano mkubwa kesho kocha Mserbia, Boris Bunjak akamuanzisha mtoto huyo wa winga wa zamani wa Yanga, Abubakar Salum ‘Sure Boy’.
    Azam jana walifanya mazoezi kwenye Uwanja wa Chamazi asubuhi na jioni wakapanda basi lao, lenye kila kitu ndani- TV, friji, choo, mziki wa maana na siti za kulala kwa safari ya takriban saa mbili kwenda Mji Kasoro Bahari, Morogoro.
    Azam imepania kushinda mechi hiyo Jumamosi ili kuiondoa Simba kileleni na kuzidi kuweka hai matumaini ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu.
    Katika kujiandaa na mechi ya Morogoro, Azam Jumanne ilicheza mechi ya kujipima nguvu na kufungwa na Simba SC mabao 3-2 katika mchezo wa kirafiki uliofanyika asubuhi kwenye Uwanja wa Chamazi, maarufu kama Azam Complex, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
    Mabao ya Simba siku hiyo yalifungwa Ramadhani Singano ‘Messi’, Uhuru Suleiman ‘Robinho’ na Daniel Akuffo, wakati ya Azam yalifungwa na Jamil Mchauru na Khamis Mcha.
    Hiyo ilikuwa mechi ya nne Azam inafungwa na Simba msimu huu katika mechi tano walizokutana hadi sasa, baada ya awali kufungwa kwa penalti kwenye fainali ya Kombe la Urafiki, kufuatia sare ya 2-2, kufungwa 2-1 kwenye Nusu Fainali ya BancABC Sup8R na 3-2 kwenye mechi ya Ngao ya Jamii, wakati wao walishinda 3-1 dhidi ya Wekundu hao wa Msimbazi, katika Robo Fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame.
    Azam na Simba zitakutana tena katika mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, mzunguko wa kwanza, Oktoba 27, mwaka huu, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.     
    Simba ndio inaongoza Ligi Kuu, hadi sasa ikiwa imeshinda mechi tano kati ya sita ilizocheza na moja tu imetoka sare, hivyo kujikusanyia pointi 16, wakati Azam inashika nafasi ya pili ikizidiwa pointi tatu, ingawa pia iko nyuma kwa mchezo mmoja.
    Mbali na Sure, wachezaji wengine wa Azam ambao bado majeruhi ni Waziri Salum, Ibrahim Jeba, wakati Samir Haji Nuhu anatumikia adhabu ya kadi hajaenda pia Morogoro sawa na Jackson Wandwi na Hamisi Mcha ‘Vialli’, ambao hawamo kabisa kwenye mipango ya kocha katika mechi hiyo. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: SURE BOY JR. SASA KAMILI KUIBEBA AZAM LIGI KUU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top