• HABARI MPYA

    Monday, October 15, 2012

    TENGA KUGOMBEA TENA URAIS TFF, NAFASI YA MAKAMU NI UTITIRI BALAA

    Rais wa TFF, Leodegar Chillah Tenga atatetea nafasi yake?

    Na Mahmoud Zubeiry
    RAIS wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Leodegar Chillah Tenga atatetea nafasi yake katika uchaguzi ujao wa shirikisho hilo, Desemba mwaka huu.
    Habari ambazo BIN ZUBEIRY imezipata kutoka kwa watu walio karibu na Tenga, zinasema kwamba awali beki huyo wa zamani wa kimataifa wa Tanzania aliamua kutogombea, lakini baada ya kushawishiwa na swahiba wake, rais wa Shirikisho la Soka la KImataifa (FIFA), Sepp Blatter sasa atagombea.
    “Tenga atagombea tena TFF, unajua Blatter ni rafiki yake na ndiye amemuomba aendelee, na Blatter mwenyewe atakuja hapa kumfanyia kampeni Tenga,”alisema mtu mmoja wa karibu na Tenga.
    Taarifa zaidi zinasema tayari Tenga amekwishaanza kuwasiliana na wapiga kura na magwiji wa kampeni kwa ajili ya uchaguzi ujao.
    Juhudi za kumpata Tenga mwenyewe kuzungumzia habari hizo hazikufanikiwa, lakini kama atagombea maana yake atachuana na Makamu wake wa sasa, Athumani Nyamlani ambaye kwa muda mrefu inaelezwa amekwishaanza kampeni.
    Upinzani zaidi kwa Tenga iwapo kweli atagombea unatarajiwa kutoka kwa Jamal Emil Malinzi, aliyekuwa mpinzani wake katika uchaguzi uliopita Desemba 14, mwaka 2008.
    Katika uchaguzi huo, Tenga alitetea nafasi yake kwa kumbwaga Malinzi kwenye ukumbi wa NSSF Waterfront kwa kura 64 dhidi ya kura 39 za Malinzi.
    Awali Malinzi alienguliwa kwa kigezo cha uzoefu, lakini akarejeshwa kuwania nafasi hiyo baada ya kushinda rufaa yake.
    Katika uchaguzi huo ulioshuhudiwa na Mwakilishi wa FIFA, Ashford Mamelodi, Athumani Nyamlani alishinda nafasi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, baada ya kujikusanyia kura 65 kati ya kura 107 zilizopigwa na kura mbili kuharibika, akimshinda Lawrence Mwalusako aliyepata kura 39 na Ali Mwanakatwe aliyeambulia kura moja.
    Nafasi ya Makamu wa Pili wa Rais, ilikwenda kwa Ramadhani Nassib aliyemwangusha mpinzani wake wa karibu, Damas Ndumbaro aliyepata kura 45.
    Baadhi ya wagombea wanaotajwa kuwania nafasi ya Makamu wa kwanza wa rais katika uchaguzi ujao ni Frederick Mwakalebela, Wallace Karia, Michael Wambura, Wakili Alex Mgongolwa, Wakili Imani Madega, Wakili Damas Ndumbaro na Lawrcence Mwalusako. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: TENGA KUGOMBEA TENA URAIS TFF, NAFASI YA MAKAMU NI UTITIRI BALAA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top