• HABARI MPYA

    Sunday, September 21, 2014

    COASTAL UNION YAREJESHA FURAHA JANGWANI, WAING’ANG’ANIA SIMBA SC 2-2 TAIFA

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    MAKOSA ya safu ya ulinzi ya Simba SC, leo yameigharimu timu hiyo kuanza na sare katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara na Coastal Union ya Tanga Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. 
    Matokeo hayo wazi yatapokewa kwa furaha na wapinzani wa jadi wa Simba SC, Yanga SC ambao jana walianza ligi kwa kichapo cha mabao 2-0 kutoka Mtibwa Sugar Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.
    Simba SC ilikwenda kupumzika ikiwa inaongoza mabao mawili, yaliyotiwa kimiani na kiungo Shaaban Kisiga ‘Malone’ na mshambuliaji, Amisi Tambwe, lakini baada ya dakika 90 matokeo yakawa 2-2.
    Karate, au soka? Kiungo wa Simba SC, Ramadhani SIngano 'Messi' katikati ya wachezaji wa Coastal, Sabri Rashid kulia na Ayoub Yahya katika mchezo wa leo

    Mabao yote ya Simba SC inayofundishwa na Mzambia, Patrick Phiri akisaidiwa na wazalendo Suleiman Matola na Iddi Pazi ‘Father’ yalitokana na jitihada za mshambuliaji wa zamani wa Yanga SC, Emmanuel Okwi.
    Kisiga alifunga bao zuri la kwanza akimtungua Shaaban mwenzake, mtoto wa mzee Hassan Kado kwa mpira wa adhabu dakika ya sita, baada ya Okwi kuangushwa nje kidogo ya boksi.
    Mfungaji bora wa msimu uliopita, Mrundi Tambwe akaanza msimu na bao kuashiria hataki kuvua ‘kiatu cha dhahabu’ baada ya kuunganisha vizuri kwa kichwa krosi ya Mganda, Okwi dakika ya 36.
    Coastal Union nao walipoteza nafasi mbili nzuri za kufunga kipindi cha kwanza, kwanza dakika ya tatu baada ya Mkenya, Itubu Imbem kuunganishia juu ya lango krosi ya Hamad Juma na baadaye Joseph Mahundi akashindwa kuunganisha krosi ya Mkenya huyo dakika ya 29.
    Bao la kwanza; Shaaban Kisiga akishangilia na Ramadhani Singano 'Messi' kushoto baada ya kufunga bao la kuongoza
    Amisi Tambwe akimtoka beki wa Coastal, Mbwana Hamisi 'Kibacha'
    Tambwe akishangilia baada ya kufunga bao la pili
    Emmanuel Okwi akimkimbiza beki wa Coastal, Sabri Rashid

    Lakini kipindi cha pili, mambo yalibadilika na Wagosi wa Kaya wakauteka mchezo. Mshambuliaji wa Uganda, Lutimba Yayo Kato aliifungia bao la kwanza Coastal dakika ya 69, akitumia udhaifu wa mabeki wa Simba SC kujisahau baada ya kiungo wao, Pierre Kwizera kuchezewa faulo.
    Mabeki wa Simba SC walitulia kumsikilizia refa Jacob Adongo wa Mara apige filimbi baada ya Kwizera kuchezewa rafu, lakini ‘akakausha’ na Yayo akafunga.
    Bao hilo, ‘liliitia ndimu’ Coastal inayofundishwa na Wakenya watatu, Yussuf Chipo, akisaidiwa na Ben Mwalala na Razack Ssiwa na kuanza kushambulia kwa kasi, ingawa Simba SC nayo iliendelea kupeleka mashambulizi langoni mwa Wagosi wa Kaya.
    Uhuru Suleiman alikosa bao la wazi dakika ya 78 baada ya kutanguliziwa pasi nzuri na Okwi, lakini akiwa amebaki na kipa Kado, akapiga juu.
    Mkenya Rama Salim aliisawazishia Coastal dakika ya 83 kwa mpira wa adhabu- baada ya beki Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ kuunawa mpira nje kidogo ya boksi.
    Mshambuliaji Paul Kiongera aliyetokea benchi kipindi cha pili alirudi nje anachechemea dakika ya 88 baada ya kuumia kufuatia kugongana na kipa Kado hivyo kumpisha Amri Kiemba.
    Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Ivo Mapunda, Miraj Adam, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Hassan Isihaka, Joseph Owino, Pierre Kwizera, Haroun Chanongo/Uhuru Suleiman dk58, Shaaban Kisiga ‘Malone’, Amisi Tambwe/Paul Kiongera dk67/Amri Kiemba dk88, Emmanuel Okwi na Ramadhani Singano ‘Messi’.
    Coastal Union; Shaaban Kado, Hamad Juma, Sabri Rashid, Abdallah Mfuko, Hamisi Kibacha, Juma Lui, Suleiman Rajab/Yayo Lutimba dk49, Razack Khalfan/Ayoub Athumani dk49, Itubu Imbem, Rama Salim na Joseph Mahundi/Abbas Athumani dk69.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: COASTAL UNION YAREJESHA FURAHA JANGWANI, WAING’ANG’ANIA SIMBA SC 2-2 TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top