![]() |
Nyosso |
RASMI, dili la Juma Said Nyosso kutua Yanga limekufa, baada ya
kujiridhisha beki huyo ni ‘Simba damu’, ila sasa mazungumzo na mshambuliaji wa
Daring Motema Pembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Mussa Hassan Mgosi
yameanza rasmi.
Kutoka ndani ya Yanga, BIN ZUBEIRY imeambiwa kwamba klabu
hiyo haina mpango kabisa wa kumsajili Nyosso na wamemtaka Mwenyekiti wa Simba,
Alhaj Ismail Aden Rage awe na amani ‘kabisaaaaaa’.
Jana BIN ZUBEIRY ilifichua kusajiliwa kwa
kipa namba mbili wa klabu ya Simba ya Dar es Salaam, Ally Mustafa Mtinge
‘Barthez’ katika klabu ya Yanga, wakati huo huo kipa Shaaban Hassan Kado
anarudishwa Mtibwa Sugar katika mkataba wa kubadilishana wachezaji baina ya
timu hizo mbili.
Mbali na Barthez Yanga pia imesajili wachezaji wengine
watatu hadi sasa, beki wa kulia Juma Abdul kutoka Mtibwa Sugar, beki wa kushoto
David Luhende kutoka Kagera Sugar, beki wa kati Kelvin Yondan kutoka Simba na
kiungo Nizar Khalfan aliyekuwa anacheza Marekani.
Usajili huu, shukrani kwao, wagombea uongozi katika uchaguzi
wa Yanga, unaotarajiwa kufanyika Julai 15, mwaka huu- Yussuf Manji anayewania Uenyekiti
na Abdallah Ahmad Bin Kleb anayewania Ujumbe pamoja na mwanachama wa klabu
hiyo, ambaye hagombei nafasi yoyote, Seif Ahmed ‘Magari’.
Aidha, Yanga inaendelea na mazungumzo na mshambuliaji Danny
Davis Mrwanda aliyekuwa anacheza Dong Tam Long An ya Vietnam, aliyewahi
kuchezea Simba SC.
Aidha, juhudi za Yanga kumpata mshambuliaji wa kimataifa wa
Uganda, Owen Kasuule zimegonga ukuta baada ya mchezaji huyo kusaini El Merreikh
ya Sudan. “Kasuule ametuambia amesaini El Merreikh, nasi tumeachana
naye,”kilisema chanzo kutoka Yanga.
Lakini Yanga bado inaendelea na jitihada za kumsajili
mshambuliaji wa kimataifa wa Rwanda, Meddie Kagere, wakati kutoka kikosi cha
msimu uliopita, wachezaji watatu wa kigeni, kipa Yaw Berko na washambuliaji
Kenneth Asamoah wote kutoka Ghana watatemwa sambamba na Davies Mwape kutoka
Zambia.
Hivi sasa Yanga inaumiza kichwa kupata beki wa kati kutoka
nje ya Tanzania atakayekuwa akisaidiana kazi na Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na
Yondan. Aidha, Yanga inafuatilia kama kweli kiungo mkabaji, Shaaban Mussa Nditi
amesaini Coastal Union ya Tanga au la ili ijaribu kumsajili.
Wachezaji wengine ambao Yanga inawatolea macho ni nyota wa
Mtibwa Sugar Said Bahanuzi ‘Ortega’ na Hussein Javu- ambao wote wana mikataba
na timu hiyo ya Manungu.
Tayari kutoka kikosi cha msimu uliopita wachezaji wazawa
Nsajigwa Shadrack, Kiggi Makassy, Bakari Mbega, Abuu Ubwa na Zuberi Ubwa wamekwishatemwa.
0 comments:
Post a Comment