• HABARI MPYA

    Wednesday, August 07, 2013

    COASTAL UNION YASAJILI MSHAMBULIAJI MGANDA KIBOKO YA SIMBA NA YANGA KUTOKA URA

    Na Princess Asia, IMEWEKWA AGOSTI 6, 2013 SAA 4:54 USIKU
    KIUNGO mshambuliaji wa URA ya Uganda, Yayo Lutimba amesaini Mkataba wa miaka miwili kujiunga na mabingwa wa zamani wa Ligi Kuu ya Bara, Coastal Union ya Tanga.
    Mkurugenzi wa Ufundi wa Coastal, Alhaj Nassor Mohamed Bin Slum ameiambia BIN ZUBEIRY leo kwamba, nyota huyo amekwishatua Tanga tayari kuanza kazi.
    Mchezaji huyo aliyejiunga na Wakusanya Kodi hao wa Uganda, Juni mwaka jana akitokea Express FC aliivutia Coastal alipokuwa na URA katika ziara ya hivi karibuni nchini Tanzania ambako alifunga mabao manne katika mechi dhidi ya Simba na Yanga Dar es Salaam, mawili kila mechi.
    Lutimba Yayo kulia akiwa na Bin Slum
    kushoto leo. Bin Slum amerejea hivi
    karibuni kutoka hija ndogo, Umrah.

    Lutimba hakuziona nyavu za Coastal wakati URA ilipomenyana na mabingwa hao wa 1988 Uwanja wa Mkwakwani, Tanga mwezi uliopita.
    Dili la kumsajili mchezaji huyo wa zamani wa kikosi cha timu ya taifa ya Uganda chini ya umri wa miaka 20 limekamilishwa leo katika hoteli ya Africana, Kampala na mwakilishi wa Coastal Union, Yusuf Akida Saad. 
    Ada ya uhamisho wa mchezaji huyo inabaki kuwa siri, ingawa URA FC imeweka kipengele cha endapo mchezaji huyo atauzwa na Coastal Union kwenda klabu yoyote hata Tanzania au nje, wao (URA SC) watapa asilimia 20.
    Mchezaji huyo aliyeipa Express FC ubingwa wa 2011/2012 anakuwa mchezaji wa pili wa URA FC kuondoka majira haya ya joto, baada ya Nahodha, Joseph Owino kujiunga tena na Simba SC wiki iliyopita.
    Uzi wa nchi; Lutimba akiwa katika jezi ya timu ya taifa ya Uganda 

    Lutimba anaungana na Waganda wengine katika Ligi ya Tanzania, ambao ni Brian Umony wa Azam, Abel Dhaira, Owino wa Simba na Hamisi Kiiza wa Yanga.
    Coastal ina Mganda mwingine, Philip Kaira ambaye amebadili uraia na kuwa Mtanzania, ambaye pia alitokea URA.
    Coastal Union ilimaliza katika nafasi ya sita kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Bara msimu uliopoita kwa pointi zake 35. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: COASTAL UNION YASAJILI MSHAMBULIAJI MGANDA KIBOKO YA SIMBA NA YANGA KUTOKA URA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top