• HABARI MPYA

    Wednesday, August 07, 2013

    SABABU TANO ZA SIMBA SC KUTULIA NA KING KIBADEN

    IMEWEKWA AGOSTI 7, 2013 SAA 12:38 ASUBUHI
    WAKATI awamu ya kwanza ya usajili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara imefungwa juzi, bado mvuto wa ligi hiyo kwa kiasi kikubwa unabakia kwa timu mbili kongwe, Simba na Yanga SC, ingawa Azam FC nayo inatazamwa, kwa sababu ndiyo mpinzani mkuu na wa kweli wa miamba hiyo.
    Kwa misimu miwili mfululizo sasa Azam sasa imeweza kuiengua moja ya klabu hizo katika michuano ya Afrika na bila shaka mwaka huu kwa maandalizi yao mazuri, wataweka tofauti kidogo katika msimu mpya.
    Misimu miwili iliyopita, Azam imekuwa ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu, kwanza nyuma ya Simba SC na baadaye nyuma ya Yanga SC na dhamira kuu ya wamiliki wa klabu hiyo msimu huu ni ubingwa.

    Ni kwa sababu hiyo nasema Azam msimu huu inaweza kuweka tofauti kutoka kuwa wa pili hadi mabingwa mbele ya Yanga au Simba. Inaweza, haimaanishi imepita, bali wana jukumu la kupigania nafasi hiyo.
    Pamoja na yote ikiwemo ujio wa wakombozi wa soka ya Tanzania, Azam FC, bado mvuto wa soka yetu kwa kiasi kikubwa unabakia kwa mahasimu hao.   
    Mara kadhaa nimewahi kuandika juu ya umuhimu wa ustawi wa klabu hizo mbili kwa sababu ndizo zinanazoteka hisia za wengi miongoni mwetu katika kupambana na viongozi mafedhuli na mafisadi ambao wanaingia kuongoza klabu hizo kwa manufaa yao.
    Na hilo haliwezi kubadilika mara moja, uimara wowote wa Azam hautabadilisha kitu kwa Simba na Yanga ni sawa tu na Manchester United na Liverpool pale England, pamoja na kwamba Wekundu wa Anfield wamefulia kwa muda sasa, bado wao kwa pamoja na Mashetani Wekundu ndiyo klabu kubwa nchini humo.
    Na uimara wa upinzani wa jadi, unatokana na uimara wa timu zote- kuwa katika hali nzuri kiushindani ili kuweza kuwavutia mashabiki wake. Tumeona msimu uliopita Simba SC wakipitia katika wakati mgumu, migogoro ikitawala katika kila nyanja.
    Wachezaji walifukuzwa, makocha walibadilishwa na uongozi ulitiwa misukosuko- hakika haikuwa hali nzuri na si vyema ikajirudia. Kitu kimoja kikubwa katika Simba na Yanga ambacho wapenzi wanajali, matokeo mazuri.
    Hawahitaji kuwa na maendeleo kama klabu nyingine mfano tu Azam FC achilia mbali TP Mazembe, bali ubingwa wa Bara na kumfunga mtani, haijalishi hata wakitolewa Raundi ya kwanza michuano ya Afrika. Mradi mpinzani kaadabishwa na taji wamechukua.
    Na kwa sababu hii, ndiyo maana Azam inawapita kama wamesimama Simba na Yanga, kwa sababu dira na malengo ni tofauti. Azam wanaumia kuona Mazembe imecheza Klabu Bingwa ya Dunia wao bado- lakini Simba na Yanga zinaoneana wivu zenyewe na ndiyo maana kila siku zinagombea wachezaji zenyewe kwa zenyewe, hazina hata ndoto za kuwa japo na Uwanja wa mazoezi. Huruma!
    Tumeiozea hali hiyo na tumekwishaandika sana sana juu ya hayo, lakini viongozi wake wameziba nta masikioni na zaidi tunaambulia kuchukiwa tu, kisa kuwaambia watu ukweli- ama kweli duniani lazima wawepo wajinga ili uwajue weledi.
    Ningependa sana kuwaasa wana Simba leo kwa ujumla- baada ya kupitia msimu mgumu, hatimaye wametulia na kuanza kuandaa timu yao upya. Viongozi wametekeleza majukumu yao vizuri kwa kuanzia kusajili, kuajiri kocha mpya, kuiweka timu kambini mapema na kuipatia mechi nyingi za kujipima nguvu.
    Kocha mzawa na gwiji wa zamani wa klabu hiyo, Abdallah Athumani Seif ‘King Kibaden’ amechukua nafasi ya Mfaransa, Patrick Liewig na amekuwa bize kuisuka timu kwa takriban miezi mitatu sasa.
    Simba SC wamemchukua Kibadeni baada ya kuvutiwa na kazi yake akiwa Kagera Sugar ambako mwishoni mwa msimu alipewa tuzo ya kocha bora wa Ligi Kuu- hakuna shaka huyu ni bora na wazi hata bila kuangalia rekodi ya msimu uliopita, Chifu Mputa ni bora.
    Ndiye huyu ambaye aliifikisha Simba SC fainali ya Kombe la CAF mwaka 1993 na wengi wanaamini alihujumiwa ndiyo maana hakuchukua taji. Usajili ambao Simba SC imepeleka TFF juzi ni uliofanywa na Kibadeni. Aliwahakiki wachezaji, akaridhia uwezo wao akabariki wasajiliwe.
    Simba SC ni kama wanaanza kujipanga upya baada ya kupitia katika msimu mgumu na wa vurugu nyingi- na mababu zetu walisema kitambo kirefu, mwanzo mgumu. Simba SC lazima kwanza watambue wapo katika hatua ya mwanzo ya kujiimarisha upya, ambayo ni ngumu, ingawa wanaweza kuwa na bahati wakapata utelezi.
    Waweke fikra zao kwamba, wanajenga timu upya na wawape muda makocha na wachezaji ili wajipange, hatimaye kufikia uwezo wa kushindana na Yanga na Azam, ambao kwa hakika wako vizuri kwa sasa zaidi yao.
    Mashabiki wawe nyuma ya timu yao kwa sasa kwa matokeo yoyote ili kuwapa moyo makocha na wachezaji wafanye kazi yao vizuri. Kuna kukosea sana tu katika hatua za mwanzoni, ila baada ya kujifunza kiasi cha kutosha, hadithi itabadilika. Dhahiri.
    Ni ngumu kufanya kazi Simba na Yanga kwa ufanisi kwa sababu ya presha ya mashabiki na hata Kibaden analijua hilo, lakini amekubali tu kujilipua kuacha kazi klabu ambayo isingemfukuza leo wala kesho na kwenda klabu ambayo anaweza kufukuzwa hata saa moja baada ya kusaini Mkataba.
    Ipo haja ya kuheshimu uwezo wa mtu, historia hata na rekodi. Kwa haya yote Kibadeni ni bora na amekwishadhihirisha hapo hapo Msimbazi si chini ya mara tatu. Anajua anachokifanya. Kikubwa tu ni kupewa sapoti na kila anayejiita Simba SC, ili hata kama si msimu ujao, basi utakaofuata atimize ndoto zake.
    Simba SC hawajui tu, lakini King Kibaden ndiye mtu ambaye anafaa kuwa kocha wao hadi atakaposema yeye mwenyewe basi. Kwanza ni Simba damu, pili ni mwalimu wa mpira kitaaluma, tatu amecheza soka na anaijua vyema, nne mzoefu kwa ujumla na tano, ni mtu mzima mwenye hekima na busara. Ramadhan Kareem.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: SABABU TANO ZA SIMBA SC KUTULIA NA KING KIBADEN Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top