• HABARI MPYA

    Saturday, September 14, 2013

    MJINI MAGHARIBI WATWAA COPA COCA COA NA KUZOA MILIONI 8, YATOA PIA MFUNGAJI BORA

    Na Mwandishi Wetu, IMEWEKWA SEPTEMBA 14, 2013 SAA 2:53 USIKU
    TIMU ya mkoa wa Mjini Magharibi (U-15), leo iliipeperusha vyema bendera ya Zanzibar kwa kuifunga Ilala bao 1-0 na kutawazwa mabingwa wapya wa mashindano ya Copa Coca Cola.
    Mchezo huo wa fainali ulichezwa uwanja wa Kumbukumbu ya Karume mjini Dar es Salaam, ambapo hadi mapumziko matokeo yalikuwa 0-0.




    Kwa ujumla pambano hilo lilikuwa gumu mno kwa timu zote mbili kwani wachezaji wake walifanya kila waliloweza kuhakikisha timu zao zinapata ushindi.
    Baada ya vuta nikuvute ya muda mrefu, wakati wa furaha kwa watoto wa RC Abdalla Mwinyi uliwadia, ambapo mchezaji machachari Yussuf Ali alifanikiwa kuandika bao pekee lililoipa Mjini Magharibi taji la pili la mashindano hayo.
    Yusuf pia, alifunga mabao yote mawili katika ushindi wa 2-0 dhidi ya Temeke kwenye mchezo wa nusu fainali uliochezwa juzi Ijumaa.
    Kwa matokeo hayo, timu hiyo imenyakua kikombe, medali za dhahabu na kitita cha shilingi milioni nane, mshindi wa pili Ilala akapewa milioni tano, na Morogoro iliyoibuka ya tatu kwa kuifunga Temeke 1-0 ikaramba shilingi milioni tatu.
    Mchezaji Juma Ali wa Mjini ameibuka mfungaji bora na kuzawadiwa shilingi laki tano. Timu hiyo inatarajiwa kurejea Zanzibar leo na mapokezi makubwa yameandaliwa na serikali ya mkoa wa Mjini Magharibi, itakapowasili bandarini.
    Hiyo inakuwa mara ya pili kwa vijana hao kutwaa ubingwa wa ngarambe hizo, ya kwanza ikiwa mwaka 2009 wakati mashindano hayo yashirikisha wachezaji walio na umri wa chini ya miaka 17.
    Mapema juzi, mara baada ya kuishinda Temeke na kutinga nusu fainali, Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Abdalla Mwinyi Khamis aliitumia salamu za pongezi timu hiyo sambamba na tunza ya shilingi laki sita.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: MJINI MAGHARIBI WATWAA COPA COCA COA NA KUZOA MILIONI 8, YATOA PIA MFUNGAJI BORA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top