• HABARI MPYA

    Saturday, October 05, 2013

    KIEMBA APAMBANISHWA NA NIYONZIMA TUZO YA MWANASOKA BORA WA GAZETI LA MWANASPOTI

    Na Mwandishi Wetu, IMEWEKWA OKTOBA 5, 2013 SAA 6:53 MCHANA
    MSHINDI wa Tuzo ya Mwanaspoti Bora wa mwaka 2013 atajulikana Novemba 8, huku nyota watano wa soka wakichuana kuwania tuzo hiyo ambayo mshindi wake atajinyakulia kitita cha Sh5 milioni.
    Wachezaji wanaowania tuzo hizo ni Amri Kiemba (Simba), Haruna Niyonzima na Kelvin Yondani (wote Yanga) Shomari Kapombe (anayechezea FC Cannes ya Ufaransa) na Themi Felix (Kagera Sugar).
    Ili kuweka usawa kwa mashabiki kuchagua wanachokitaka, wachezaji hao wanapigiwa kura na mashabiki kwa kuandika ujumbe mfupi unaoanza na neno KURA kisha jina la mchezaji anayemchagua kati ya hao waliotajwa na kisha kutuma kwenda namba 15678.
    Amri Kiemba atachuana na Haruna Niyonzima kuwania tuzo ya Mwanaspoti 

    Meneja Masoko wa Kampuni ya Mwananchi Communications ambao ndio wachapishaji wa Gazeti la Mwanaspoti, Bernard Mukasa alisema: “Tuzo hii inatambulika kama Tuzo ya Mwanaspoti Bora wa Soka Tanzania 2013 na inadhaminiwa na Kampuni ya Simu ya Vodacom Tanzania kama mdhamini mkuu pamoja na Clouds FM.”
    “Ni tuzo ya kipekee na ya kwanza kabisa nchini kwa sababu inashirikisha wachezaji wengi wanaowania tuzo hiyo na mashabiki wote wa soka wana fursa ya kupiga kura na kuamua nani ni bora. Kwa mwaka huu licha ya kumpata Mwanaspoti Bora wa soka wa mwaka pia kutakuwa na vipengele vingine zaidi ya 10 ikiwemo kocha bora, mwamuzi bora, mchezaji bora wa kike, mchezaji bora chipukizi, kikosi bora, mchezaji bora wa kigeni, mchezaji bora wa Tanzania anayecheza nje ya nchi. Kuna kipengele kingine kipo lakini tutakitambulisha siku hiyohiyo na kila mtu atapigwa na butwaa,”alisisitiza Mukasa.
    Haruna Niyonzima atapambana na Amri Kiemba tuzo ya Mwanaspoti

    Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano wa Vodacom Tanzania, Joseline Kamuhanda alisema: “Vodacom tumeendelea kuwa nguzo muhimu katika maendeleo ya soka la Tanzania, sasa soka limekuwa zaidi ya burudani kwa Watanzania kutokana na chachu ambayo tumeiweka tangu tuanze kudhamini Ligi Kuu.”
    “Licha ya kutambua kuwa soka ni burudani tumeamua kudhamini tuzo hizi ili kuendelea kuwa sehemu ya mafanikio ya soka Tanzania na kuleta mapinduzi katika soka kwa kutambua mchango wa wachezaji mbalimbali ambao mpira kwao ni ajira kuu,” alisema Kamuhanda. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: KIEMBA APAMBANISHWA NA NIYONZIMA TUZO YA MWANASOKA BORA WA GAZETI LA MWANASPOTI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top