• HABARI MPYA

    Saturday, October 05, 2013

    YANGA SC KUMKOSA NIYONZIMA KESHO IKIMENYANA NA MTIBWA SUGAR, DIDA NAYE LABDA

    Na Mahmoud Zubeiry, IMEWEKWA OKTOBA 5, 2013 SAA 7:57 MCHANA
    KIUNGO tegemeo wa Yanga SC, Haruna Hakizimana Fadhil Niyonzima ameomba mapumziko ya siku ‘mbili tatu’ kutokana na matatizo ya kifamilia yanayomkabili kwa sasa, maana yake hatakuwemo kwenye kikosi cha timu yake kitakachomenyana na Mtibwa Sugar kesho Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Ofisa Habari wa Yanga SC, Baraka Kizuguto ameiambia BIN ZUBEIRY leo kwamba, Niyonzima hajashiriki mazoezi ya Yanga tangu kuunguliwa na nyumba anayoishi Magomeni Makuti, Dar es Salaam, usiku wa kuamkia juzi (Oktoba 3, 2013) na kusababisha hasara ya vitu kadhaa. 
    Mapumziko; Haruna Niyonzima amepewa mapumziko baada ya matatizo ya kifamilia

    Pamoja na hayo, imeripotiwa pia mchezaji huyo wa kimataifa wa Rwanda, amefiwa na mtoto wake nchini Uganda, aliyekuwa akiishi na mama yake huko. Dar es Salaam Niyonzima anaishi na mkewe na mtoto wake mwingine.
    Kizuguto amesema klabu inafikiria namna ya kumsaidia Niyonzima baada ya matatizo hayo ili aishi kwa usalama, aweze kuitumikia myema klabu hiyo.
    Mbali na Niyonzima, Kizuguto amesema kwamba kipa Deo Munishi ‘Dida’ aliyeumia mazoezini jana, naye leo hakufanya mazoezi, maana yake yupo kwenye hatihati kushiriki mchezo wa kesho.
    Dida aliumia jicho baada ya kugongana na beki Rajab Zahir katika mazoezi ya timu hiyo Uwanja wa sekondari ya Loyola, Mabibo, Dar es Salaam jana.  
    Nyumba ya Niyonzima imeungua zaidi eneo la sebuleni na fenicha zote, Teleisheni na Redio vimeteketea kwa moto.
    Janga hilo lilitokea wakati mchezaji mwenyewe akiwa ndani ya nyumba yake na kama si jitihada za majirani kujitokeza kumsaidia kuzima moto huo, athari zingekuwa kubwa.
    Nyumba hiyo ina wapangaji wawili na upande ulioathirika kwa moto ni ambao anaishi mchezaji huyo tu.
    Yanga SC inashuka dimbani kesho kumenyana na Mtibwa katika mfululizo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, huo ukiwa mchezo wa saba baada ya kushinda mechi mbili tu kati ya sita, sare tatu na kufungwa moja.
    Yanga SC ambao ndiyo mabingwa watetezi, wanazidiwa pointi tano na Simba SC iliyo kileleni.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: YANGA SC KUMKOSA NIYONZIMA KESHO IKIMENYANA NA MTIBWA SUGAR, DIDA NAYE LABDA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top