• HABARI MPYA

    Saturday, October 05, 2013

    SIMBA SC YAPUNGUZWA KASI NA WATOTO WA MKWASA, AZAM NA COASTAL HAKUNA MBABE

    Na Waandishi Wetu, IMEWEKWA OKTOBA 5, 2013 SAA 12:05 JIONI
    LIGI Kuu ya Vodacom Tanzania Bara imeendelea leo, huku vinara Simba SC wakipunguzwa kasi kwa sare ya 1-1 na Ruvu Shooting Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na Azam pia wakitoka sare ya bila kufungana na Coastal Union Uwanja wa Mkwakwani, Tanga. 
    Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Simba SC ililazimika kusubiri hadi dakika ya 51 kupata bao la kusawazisha kwa penalti kupitia kwa Amisi Tambwe, kufuatia Betram Mombeki kuangushwa kwenye eneo la hatari, baada ya Ruvu Shooting kutangulia kufunga dakika ya nane kupitia kwa Said Dilunga.
    Beki wa Coastal Union, Juma Nyosso akimdhibiti mshambuliaji wa Azam FC, John Bocco 'Adebayor' katika mchezo wa leo, Uwanja wa Mkwakwani.

    Hata hivyo, wachezaji wa Ruvu Shooting walimzonga refa Mohamed Theophil wakipinga penalti hiyo, kabla ya kulainika na kukubali ipigwe- na Mrundi Tambwe akaenda kufunga bao lake la nane ndani ya mechi saba katika msimu wake wa kwanza Simba SC.
    Matokeo hayo, yanaifanya Simba SC itimize pointi 15 baada ya mechi saba na kuendelea kushikilia usukani wa Ligi Kuu.
    Uwanja wa Mkwakwani, Tanga mechi ilikuwa kali, ilitawaliwa na vurugu za mashabiki tangu hata kabla mchezo haujaanza. 
    Kosa kosa zilikuwa za pande zote mbili, safu ya ushambuliaji ya Coastal ikiongozwa na Mganda, Yayo Lutimba na Pius Kisambale na Azam ikiongozwa na John Bocco, Mganda Brian Umony na Kipre Tchetche wa Ivory Coast.
    Biashara inalipa; Mrundi Amisi Tambwe ameendelea kuibeba Simba SC

    Refa Andrew Shamba aligeuka kituko kipindi cha pili, baada ya kuwapa kona isiyostahili Azam na ilipopigwa wakafanikiwa kupata bao, lakini akakataa bao hilo.
    Baada ya kutoa kona hiyo, beki wa Azam Erasto Nyoni alienda kupiga vizuri ikaunganishwa nyavuni na John Bocco kwa kichwa dakika ya 71, lakini Shamba akaamuru mpira uwekwe chini upigwe kuelekea lango la Azam- kana kwamba kuna faulo ilichezeka.
    Mshika kibendera namba mbili, Hassan Zani alisababisha mchezo kusimama kwa dakika tatu ili apatiwe huduma ya kwanza, baada ya kupigwa chupa na mashabiki wa Coastal Union dakika ya 43.
    Beki wa kulia wa Coastal Union, Hamad Hamisi alitolewa nje kwa kasi nyekundu dakika ya 70 baada ya kumpiga kichwa Kipre Tchetche wa Azam FC. Tukio hilo lilifuatia  majibizano na kusukumana kwa wachezaji hao.
    Mshambuliaji wa Azam, Kipre Tchetche alikutana na ‘mvua’ ya chupa dakika ya 73 akiambaa kuelekea langoni mwa Coastal Union, jambo ambalo lilimfanya refa asimamishe mchezo na kuomba Polisi waende kusimama mbele ya jukwaa la mashabiki wa Coastal.
    Baada ya mchezo huo, mashabiki wa Coastal walitoka jukwaani na kuwafuata marefa, lakini Polisi walifanikiwa kuwadhibiti. Hadi BIN ZUBEIRY inaondoka Uwanja wa Mkwakwani, marefa walikuwa bado hawajatoka na Polisi walikuwa wameweka ulinzi.
    Kikosi cha Coastal Union kilikuwa; Shaaban Kado, Hamad Hamisi, Othman Tamim, Mbwana Hamisi ‘Kibacha’, Juma Nyosso, Jerry Santo, Uhuru Suleiman/Yussuf Chuma dk79, Crispin Odula, Pius Kisambale/Suleiman Kassi ‘Selembe’ dk64, Yayo Lutimba na Keneth Masumbuko.
    Azam FC; Mwadini Ally, Erasto Nyoni, Waziri Salum, Said Mourad, Aggrey Morris, Kipre Balou, Brian Umony/Seif Abdallah dk69, Salum Abubakar, John Bocco, Humphrey Mieno na Kipre Tchetche.Katika mechi nyingine, Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha, JKT Oljoro imelala 2-1 mbele ya Mbeya City. 
    Mabao ya Mbeya yalifungwa na Paul Nonga dakika ya 21 na Peter Mapunda dakika ya 84, wakati la Oljoro lilifungwa na Expedito Kiduko dakika ya 77.
    JKT Ruvu imeifunga Kagera Sugar mabao 2-1 Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam. Mabao ya Ruvu yamefungwa na Salum Machaku dakika ya nane na Bakari Kondo dakika ya 69, wakati la Kagera limefungwa na Themi Felix dakika ya 67. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: SIMBA SC YAPUNGUZWA KASI NA WATOTO WA MKWASA, AZAM NA COASTAL HAKUNA MBABE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top