• HABARI MPYA

    Wednesday, January 08, 2014

    CXC KUWAZAWADIA KIPA BORA, MFUNGAJI BORA NA MCHEZAJI BORA KOMBE LA MAPINDUZI

    Na Mahmoud Zubeiry, Zanzibar
    KAMPUNI ya CXC Safaris & Tours itatoa zawadi kwa wachezaji watatu kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi, inayoendelea visiwani hapa, ambao ni mchezaji bora, mfungaji bora na kipa bora.
    Mkurugenzi wa Kampuni ya CXC inayosifika kwa huduma nzuri za kitalii nchini, Charles Hamkah ameiambia BIN ZUBEIRY leo kwamba ametoa ofa hiyo kwa Kamati ya Kombe la Mapinduzi, ili kunogesha michuano hiyo.
    “Nimeamua kutoa ofa hii ili kunogesha mashindano haya, ambayo kwa kweli yanastahili kuungwa mkono zaidi ili yawe makubwa na bora zaidi,”alisema.
    Mfano wa kuigwa; Mkurugenzi wa CXC Safaris & Tours, Charles Hamkah atatoa zawadi kwa mfungaji bora, kipa bora na mchezaji bora Kombe la Mapinduzi

    Hamkah amewaomba wadau wengi zaidi kujitokeza kupiga jeki zaidi mashindano hayo ambayo yanaendelea vyema tangu yaanzishwe mwaka 2007.
    Kuhusu zawadi, Hamkah alisema atakutana na Kamati ya Kombe la Mapinduzi kujadiliana nayo viwango, lakini amesema zitakuwa zawadi nzuri na wachezaji watakaoshinda watazifurahia.
    Hadi sasa, wachezaji sita wanachuana vikali katika ufungaji wa mabao, ambao ni Owen Kasuule, Feni Ali wote wa URA ya Uganda, ambao kila mmoja ana mabao matatu, Amri Kiemba Simba SC mabao mawili sawa na Brian Umony wa Azam FC, Mwinyi Mngwali wa Chuoni na Herman Waswa wa KCC.
    Waliofunga bao moja kila mmoja ni Tony Odur, Stephen Bengo, Masiko Tom, William Waoro wa KCC ya Uganda, Hamisi Ali, Maulid Ibrahim Kapenta wa KMKM, Deus Kaseke, Paul Nonga wa Mbeya City, Ahmed Ali Omar, Mohamed Juma wa Cloves Stars, Joshua Oyoo, Ismail Dunga, Clifford Alwanga wa Tusker FC ya Kenya, Himid Mao, Kipre Tchetche wa Azam FC, George Thomas, Shaaban Moke wa Chuoni, Ekee Brayton Obina wa Ashanti na Abdallah Seif Bausi wa Spice Stars.
    Hawafungiki; Ivo Mapunda wa Simba SC (juu) na Mwadini Ali wa Azam FC (chini) wanachuana kuwania tuzo ya kipa bora Kombe la Mapinduzi, hadi sasa wakiwa hawajaruhusu nyavu zao kuguswa
    Kwa upande wa makipa ambao wanafanya vizuri zaidi hadi sasa ni Ivo Mapunda wa Simba SC ambaye amedaka mechi mbili bila kufungwa na Mwadini Ali wa Azam, ambaye amedaka mechi tatu bila kufungwa. 
    Yaw Berko wa Simba SC pia hajafungwa, lakini amedaka mechi moja tu na ambayo inaweza ikawa mechi yake ya mwisho ya mashindano haya, kwani katika hatua ya mtoano Ivo anapewa nafasi kubwa zaidi ya kudaka.  
    Wachezaji ambao wameonyesha viwango vya hali ya juu hadi sasa kwenye mashindano haya ni Salum Abubakar ‘Sure Boy’ wa Azam, Ramadhani Singano ‘Messi’ wa Simba SC, Ismail Dunga wa Tusker, Stephen Bengo wa KCC, Owen Kasuule wa URA, Mwinyi Mngwali wa Chuoni na Maulid Ibrahim Kapenta wa KMKM. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: CXC KUWAZAWADIA KIPA BORA, MFUNGAJI BORA NA MCHEZAJI BORA KOMBE LA MAPINDUZI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top