• HABARI MPYA

    Friday, January 17, 2014

    JESSICA JACKSON: KINDA MWENYE KIPAJI CHA AJABU NETIBOLI

    Na Zaituni Kibwana, aliyekuwa Zanzibar
    “Naupenda sana mchezo wa netiboli na ndoto zangu ni kupeperusha bendera ya nchi yangu kimataifa,” Hivyo ndivyo alivyoanza kusema mchezaji chipukizi wa timu ya Netiboli maarufu kama ‘Kilimanjaro Queens’,  Jessica Jackson.
    Jessica au Jeska kwa urahisi kutamka, aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na BIN ZUBEIRY kwenye michuamo ya Kombe la Mapinduzi yaliomalizika hivi karibuni  visiwani Zanzibar huku Uganda ikinyakuwa ubingwa wa  jumla.
    Chipukizi huyo aliyechaguliwa kwa mara ya kwanza kwenye kikosi hicho kinachonolewa na Winnie Emmanuel  alizungumzia historia yake na namna alivyojikita kwenye mchezo huo.
    Mtoto Jessica, kinda mwenye kipaji cha ajabu Netiboli
    Jessica katika mahojiano na Mwandishi na makala haya, Zaituni Kibwana

    Bila kusita mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 15  huku akicheza nafasi ya Center na WA alisema kuwa alianza kucheza mchezo huo akiwa chini ya timu ya Kijichi Qeens.
    Timu hiyo iliyokuwa ikifundishwa na baba yake Jackson Hezron iliweza kukuza kipachi chake na kuweza kuwa mchezaji tishio.
    Jeska ambaye kwa sasa anasoma kidato cha tatu kwenye shule ya St Mary Kitende nchini Uganda alisema kuwa alichaguliwa timu ya taifa baada ya kufanya vema kwenye michuano ya Taifa Cup akiwa na timu ya Kinondoni.
    Chipukizi huyo aliyezaliwa Agosti 25 mwaka 1998 alisema kuwa uwepo wake kwenye timu hiyo ya Taifa umeweza kufikisha ndoto zake za kuonekana kimataifa.
    Bila kusita, Jeska alisema kuwa alijifunza mchezo huo ili siku moja aweze kupeperusha bendera ya Taifa ulimwenguni.
    “Mimi naamini nina uwezo wa hali ya juu hivyo naamini ipo siku na mimi nitaweza kuitangaza nchi yangu kwenye michuano ya kimataifa,”alisema.
    Jessica kulia akiichezea Taifa Queens dhidi ya Kenya Kombe la Mapinduzi
    Jessica katika kikosi cha Taifa Queens

    Jeska aliyechukuliwa na shule ya vipaji ya Makongo Sekondari alipohamishwa kutokana na kipaji chake baada ya kufaulu shule ya Mtoni Relini alisema kuwa anapambana na changamoto nyingi kwenye ndoto zake hizo.
    “Huu mchezo ni wa kujitolea hivyo kuna changamoto nyingi sana ikiwemo kukosa mechi za kirafiki za kujihakikishia uwezo wangu,”alisema
    Alipotakiwa kutaja faida za mchezo huo ni pamoja na kuzunguka nchi mbalimbali ikiwemo nchi za Afrika Mashariki kama Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi.
    Jeska ambaye ni Msukuma alisema amerithi mchezo huo kutoka kwa mama yake Paulina Msingi ambaye anaendelea kumpa mbinu mbalimbali za kujiendeleza.
    Chipukizi huyo anayevutiwa na GD wa timu ya Taifa Lilian, aliwataka vijana wenzake kujifunza mchezo huo.
    “Huu mchezo ni mzuri na una faida nyingi sana hivyo tujitolee kujifunza mchezo huu kwa kuwa Tanzania kuna vipaji naamini,”alisema
    Jeska ambaye kwa sasa anacheza kwenye timu ya Smask Qeen Kampala aliwataka watanzania na wapenda mchezo huo kujitokeza kudhamini Chama Cha netiboli Tanzania CHANETA ili kuweza kuandaa mashindano mengi.
    “Unajua kukiwa na mashindano sisi vijana ndio tunaonekana, na Chaneta haina fedha hivyo watau wawasadie,”alisema
    Licha ya Jeska kuyasema hayo kocha wake Winnie  alimwangia sifa chipukizi huyo na kusema kuwa atafika mbali zaidi.
    “Jeska anapenda kujifunza, akikosea anauliza tungekuwa na vijana kama hawa angalau 15 Tanzania tusingekamatika,”alisema
    Kocha huyo hakusita kuwapa ushauri wazazi wengine kuwa wainge mfano wa kina Jeska kwani wameweza kutoa kipaji kinachosaidia Taifa.
    “Wazazi wakina Jeska wanaitaji pongezi kubwa sana kwani wamezalisha kipaji kukubwa sana ambacho kinasaidia,”alisema
    Alisema kuwa chama chao kina changamoto kubwa kutokana na uchache wa timu,  kutokana na kutokuwa na vipaji.
    Tuna msukumo wa kuzalisha vijana wapya nchini kwenye mchezo huo ambao mara kwa mara yanapotokea mashindano kama ya taifa, ligi daraja la kwanza na mengine ya kitaifa wachezaji ni walewale tuliozoea kuwaona tangu miaka ya 2000 ndiyo wanaoitwa kwenye timu ya taifa.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: JESSICA JACKSON: KINDA MWENYE KIPAJI CHA AJABU NETIBOLI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top