• HABARI MPYA

    Thursday, January 09, 2014

    TAMBWE AMPOKONYA BAO MESSI, ASEMA AMEFUNGA YEYE

    Na Mahmoud Zubeiry, Zanzibar
    MSHAMBULIAJI wa Simba SC, Amisi Tambwe amesema kwamba bao la pili la timu hiyo katika ushindi wa 2-0 dhidi ya Chuoni ya Unguja kwenye Robo Fainali ya Kombe la Mapinduzi jana Uwanja Amaan, Zanzibar alifunga yeye na si Ramadhani Singano ‘Messi’.
    Tambwe alisema kwamba Messi alitia krosi tu ambayo yeye aliiunganisha nyavuni, lakini akashangaa uwanjani kutangazwa amefunga Singano.
    Lakini Washkaji; Messi na Tambwe wanagombea bao la pili la Simba jana

    “Nimefunga mimi, lile ni bao langu jamani, siyo Messi”alisema Mrundi huyo, ambaye ukiondoa bao hilo analogombea, ambalo tayari amepewa Messi, hajafunga kwenye mashindano haya hadi sasa.
     IIlivyoonekana jana, mpira uliopigwa na Messi kutoka wingi ya kulia ulikatwa na upepo wakati unaelekea kwa Tambwe na kutinga moja kwa moja nyavuni kuipatia Simba SC bao la pili.   
    Jana ulikuwa ni usiku mwingine wa nyota ya mjukuu wa mzee Singano kung’ara akiwa na jezi na Wekundu wa Msimbazi. 
    Kwa ushindi huo, Simba SC itamenyana na URA ya Uganda katika Nusu Fainali ya pili keshokutwa Uwanja wa Amaan, Saa 2:00 usiku, baada ya Azam na KCC zitakazomenyana Saa 10:00 jioni. 
    Messi alifunga bao la kwanza dakika ya 47 kwa shuti kali baada ya kukutana na krosi ya Issa Rashid ‘Baba Ubaya’ kutoka wingi ya kushoto.
    Bao la pili, analogombea na Tambwe, Messi alifunga dakika ya 59 baada ya kupiga mpira kutokea pembeni kulia na kuwachanganya mabeki wa Chuoni kisha kuzama nyavuni. 
    Pamoja na kufunga mabao hayo mawili, Messi alicheza kwa kiwango cha juu jana na haikushangaza alipotajwa kuwa mchezaji bora wa mechi baada ya mchezo huo na kuzawadiwa king’amuzi cha Azam TV.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: TAMBWE AMPOKONYA BAO MESSI, ASEMA AMEFUNGA YEYE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top