Azam FC |
Na Mahmoud Zubeiry
AZAM FC leo jioni
watafanya mazoezi kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya, ili kuuzoea kabla ya
mechi ya kesho dhidi ya wenyeji, Prisons katika mfululizo wa Ligi Kuu ya
Vodacom Tanzania Bara.
Mabingwa hao
wa Kombe la Mapinduzi na washindi wa pili wa Klabu Bingwa Afrika Mashariki na
Kati, Kombe la Kagame wapo mjini Mbeya tangu juzi saa 1:00 usiku na jana
walifanya mazoezi kwenye Uwanja wa sekondari ya Iyunga mjini humo.
Kikosi kizima
cha Azam kipo vizuri kuelekea mchezo unaitarajiwa kuwa mgumu kwao na wachezaji
wa morali ya ushindi, ili kuweka vizuri mazingira ya kutwaa taji la kwanza la
ubingwa wa Ligi Kuu ya Bara.
Azam
waliondoka Morogoro juzi asubuhi baada ya mechi yao na Polisi kwenye Uwanja, Jamhuri
Jumamosi ambayo walishinda 1-0, bao pekee la mshambuliaji kutoka Ivory Coast,
Kipre Herman Tchetche.
Mbeya ni
kati ya vituo ambavyo vinawaogopesha vigogo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania
Bara, Azam, Simba na Yanga kutokana na imani kwamba Prisons haifungiki kwenye
Uwanja wake.
Sababu kubwa
ni ubovu wa Uwanja wa Sokoine, ambao wenyewe Prisons wameuzoea na wanaujulia,
wakati timu nyingine hupata tabu mno.
Kati ya
vigogo hao watatu, ambao wanafukuzana kuwania ubingwa wa Ligi Kuu, Azam inakuwa
timu ya pili kwenda Mbeya, baada ya Yanga iliyolazimishwa sare ya bila
kufungana na Wajelajela hao kwenye mechi yao ya kwanza ya ligi hiyo.
Simba
imeanzia Dar es Salaam kucheza na Prisons, Septemba 29, mwaka huu katika mechi
ambayo walishinda kwa taabu mabao 2-1 na sasa watarudiana na Wajelajela hao
mjini Mbeya katika mzunguko wa pili wa ligi hiyo.
Mikoa
mingine tishio ni Kanda ya Ziwa, ambako Azam tayari imekwishamaliza na
kukusanya pointi nne baa ya kuifunga 1-0 Kagera Sugar Uwanja wa Kaitaba kabla
ya kulazimishwa sare ya 2-2 na Toto Africans Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
Yanga pia
imemaliza deni la Kanda ya Ziwa, ikiambulia pointi tatu, baada ya kufungwa 1-0
na Kagera na kushinda 3-1 dhidi ya Toto.