• HABARI MPYA

    Tuesday, October 16, 2012

    NGASSA AANZA KUJIFUA NA SIMBA, LAKINI ASEMA HALI YAKE BADO TETE

    Ngassa

    Na Mahmoud Zubeiry
    MRISHO Khalfan Ngassa ameanza mazoeizi jana timu yake Simba SC kwenye Uwanja wa Kinesi, Urafiki, Dar es Salaam, lakini amesema bado hayuko sawa sawa, maana yake uwezekano wa kucheza mechi ya kesho dhidi ya timu yake ya zamani, Kagera Sugar Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ni mdogo.
    Akizungumza na BIN ZUBEIRY jana, Ngassa ambaye aliugua Malaria baada ya mechi dhidi ya Yanga, Oktoba 3, mwaka huu alisema kwamba bado anahisi hana nguvu.
    “Nimeanza mazoezi na timu, lakini hata hivyo bado hali yangu haiko sawa sawa kwa kweli, najisikia mwili hauna nguvu, hii Malaria ilinipelekesha sana, ila najikongoza hivyo hivyo,”alisema Ngassa.
    Kiungo mwingine wa Simba SC aliyekuwa anaumwa Malaria, Ramadhani Chombo ‘Redondo’ naye ameanza mazoezi na timu na anaweza kucheza kesho.  
    Mbali na Redondo, katika mchezo huo, Simba inatarajiwa kuwapokea wachezaji wake wengine watatu iliyowakosa kwenye mechi iliyopita dhidi ya Coastal Union Jumamosi Uwanja wa Mkwakwani, Tanga ambayo iliisha kwa sare ya bila kufungana, Emmanuel Okwi aliyekuwa kwao Uganda kuichezea timu yake ya taifa, Komabil Keita, Haruna Shamte na Kiggi Makasy waliokuwa majeruhi.
    Mechi nyingine za kesho zitakuwa kati ya Prisons na Azam FC kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya, Polisi Morogoro na JKT Ruvu Uwanja wa Jamhuri, Morogoro, Mgambo JKT na Toto Africans Uwanja wa Mkwakwani, Tanga na JKT Oljoro dhidi ya African Lyon Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha.
    Simba bado ipo kileleni mwa Ligi Kuu kwa pointi zake 17, baada ya kucheza mechi saba, ikifuatiwa na Azam FC yenye pointi 16, ambayo hata hivyo imecheza mechi sita, wakati Yanga inashika nafasi ya tatu kwa pointi zake 11, baada ya kucheza mechi saba pia. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: NGASSA AANZA KUJIFUA NA SIMBA, LAKINI ASEMA HALI YAKE BADO TETE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top