• HABARI MPYA

    Tuesday, October 16, 2012

    YANGA SC SASA KUINGIA KAMBINI LEO BAADA YA KUKWAMA JANA

    Wachezaji wa Yanga wakipasha

    Na Mahmoud Zubeiry
    KIKOSI cha Yanga kinatarajiwa kuingia kambini leo katika hoteli ya Uppland, Changanyikeni, Dar es Salaam kujiandaa na mchezo wao ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Ruvu Shooting Jumamosi wiki hii kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Yanga ilikwama kuingia kambini jana ilivyopanga na badala yake sasa wataingia leo Changanyikeni, ili kuziweka fikra za wachezaji pamoja kuelekea mechi hiyo ya Jumamosi.
    Habari njema ni kwamba, beki Kevin Yondan jana alianza mazoezi mepesi kwenye Uwanja wa sekondari ya Loyola, Dar es Salaam, ikiwa ni mara ya kwanza tangu agongwe na kiungo wa Simba, Haruna Moshi ‘Boban’ katika mechi baina ya wapinzani hao wa jadi, Oktoba 3, mwaka huu.
    Pamoja na Yondan, mshambuliaji Said Bahanuzi aliyekuwa anasumbuliwa na maumivu ya nyama za paja naye alianza pia mazoezi mepesi jana kwenye Uwanja wa sekondari ya Loyola, Dar es Salaam.
    Bahanuzi ‘Spider Man’ alichanika nyama za paja la mguu wa kulia katika mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba Jumatatu wiki iliyopita.
    Bahanuzi aliumia dakika ya 23, baada ya kugongana na beki Benjamin Effe wa Kagera Sugar na kushindwa kuendelea na mchezo, nafasi yake ikichukuliwa na Jerry Tegete katika mechi ambayo Yanga ililala 1-0, beo pekee la Themi Felix.
    Bahanuzi ndiye tegemeo la mabao la Yanga kwa sasa, kwani tangu ajiunge na timu hiyo akitokea Mtibwa Sugar msimu huu, ameifungia mabao 12 katika mechi 13, ikiwemo ile dhidi ya Kagera aliyocheza kwa dakika 23 kabla ya kuumia na kutoka. 
    Yanga kwa sasa inashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu kwa pointi zake 11, baada ya kucheza saba, kushinda tatu, sare mbili na kufungwa mbili.
    Simba iliyocheza mechi saba pia, inaongoza ligi hiyo kwa pointi zake 17, ikifuatiwa na Azam FC yenye pointi 16, iliyocheza mechi sita.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: YANGA SC SASA KUINGIA KAMBINI LEO BAADA YA KUKWAMA JANA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top