![]() |
AMEBWAGA MANYANGA; Julio kuli akila bata zake Leaders Club |
INGAWA Coastal Union ya sasa inaonekana kuwa vizuri kifedha na inafanya usajili wa kupambana msimu ujao, lakini hiyo haijamzuia kocha Jamhuri Mussa Kihwelo 'Julio' kuacha kazi. Coastal Union sasa inamchukua kocha wa Bandari FC ya Kenya, Hamisi Shedu kurithi mikoba Julio, beki wa zamani wa Simba SC, Plisner na CDA ya Dodoma. Mwenyekiti wa timu hiyo, Ahmed Aurora alisema jana; "Tumefika katika hatua nzuri na Shedu (Hamis) kuja Tanzania kuifundisha timu yetu kwa msimu ujao wa Ligi Kuu Bara." Alisema; "Mkataba wetu na Julio (Jamhuri) umemalizika na yeye binafsi amesema anahitaji kujiweka pembeni kuendelea na majukumu mengine ya kitaifa." "Bado tulihitaji kuendelea naye, lakini hatuna budi kuheshimu uamuzi wake, ni kocha ambaye tutaendelea kumkumbuka ndani ya klabu yetu kwa mazuri yote aliyofanya kuitoa Coastal mkiani mwa ligi hadi kumaliza nafasi ya tano." alisisitiza. Aurora alisema ujio wa Julio kwenye timu hiyo uliamsha morali kwa wachezaji na timu hiyo kufanya vizuri hatua yote ya mzunguko wa pili na kuinusuru kushuka daraja. "Aah! Shedu (Hamis) anatarajia kutua nchini wakati wowote kuanzia sasa kwa ajili ya kukinoa kikosi chetu, tutampa kwanza mkataba wa miezi sita kuangalia uwezo wake kama tulivyofanya kwa Julio." Alisema endapo atafaulu mtihani huo wataingia naye mkataba wa miaka miwili wa kuifundisha timu hiyo. Kocha huyo aliwahi kuifundisha Coastal Union ya Tanga miaka ya nyuma kwa mafanikio makubwa. |
0 comments:
Post a Comment