• HABARI MPYA

    Sunday, June 10, 2012

    TENGA AWAFARIJI SIMBA KUHUSU YONDAN

    Yondan akisaini Yanga wiki hii
    KLABU ya soka ya Simba imepokea kwa furaha taarifa kwamba Rais wa Shirikisho la Mpira was Miguu Tanzania (TFF), Leodger Chila Tenga, ameagiza kufanyika kwa uchunguzi kuhusiana na namna mchezaji wa Simba na Taifa Stars, Kelvin Patrick Yondani, alivyoondoka kambini usiku wa kuamkia Juni 7 mwaka huu.
    Ofisa Habari wa klabu ya Simba, Ezekiel Kamwaga ameiambia BIN ZUBEIRY usiku huu kwamba, katika barua ambayo Tenga ameiandikia Simba, ameahidi kwamba uchunguzi utafanyika katika maeneo makuu mawili. 
    Ameyataja maeneo hayo kuwa  iwapo ni kweli Yondani aliondoka kambini usiku, pili iwapo aliondoka kwa ruhusa maalumu au alitoroka. Tenga ameahidi kwamba kama ikibainika kwamba aliondoka bila ruhusa, basi hatua zitachukuliwa kwa wote waliohusika chini ya taratibu za maadili kwa wachezaji  (Players Code of Conduct).
    Kamwaga amesema kutokana na kauli hiyo ya Tenga, uongozi wa Simba umeamua sasa kwamba hautozungumza lolote kuhusiana na masuala ya Yondani na tayari wamewasilisha vielelezo vyake TFF na kote kwingine ambako suala hilo linaweza kufika na kilichobaki sasa ni kusubiri vyombo husika vifanye kazi yake.
    Amesema Simba SC inapenda kuwaomba wapenzi na wanachama wake kutulia na kutobabaishwa na taarifa za wachezaji wake kusajiliwa na timu nyingine. "Kwa sasa Simba inaendelea na mikakati yake ya usajili unaokidhi vigezo vya kimataifa, ambao ulisababisha msimu uliopita itwae ubingwa wa Tanzania na kuifunga YANGA goli 5-0,"alisema.
    Amesema Simba si timu ya maneno mengi kwenye usajili bali ni vitendo. "Tunaomba wanachama wetu watulie na mara ifikapo tareje Juni 15, mwaka huu, mbivu na mbichi zote zitajulikana. Siku hiyo, Simba itatangaza wachezaji wake wote iliyowasajili na iliyowaacha,"alisema. 
    Amesema Simba ndiyo mabingwa wa Tanzania na washabiki wake wanatakiwa kutembea vifua mbele popote pale walipo na wasichanganywe na taarifa za pembeni na uongozi uko makini na unafanya kazi zake kisayansi.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: TENGA AWAFARIJI SIMBA KUHUSU YONDAN Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top