• HABARI MPYA

    Thursday, October 03, 2013

    NDITI MAMBO 'SUPA' CHELSEA, NDOTO ZA KUCHEZA LIGI KUBWA ULAYA KARIBU KUTIMIA

    Na Prince Akbar, IMEWEKWA OKTOBA 3, 2013 SAA 11:33 JIONI
    KIUNGO chipukizi Mtanzania, Adam Nditi amepandishwa kutoka timu ya akademi ya Chelsea ya England hadi timu ya vijana chini ya umri wa miaka 21- maana yake akifanya vizuri wakati wowote anaweza kupandishwa rasmi kikosi cha kwanza.
    Tayari dalili za Nditi kupandishwa kikosi cha kwanza cha The Blues zimeanza kutokana na mara kadhaa kushirikishwa kwenye mazoezi ya kikosi hicho baada ya ujio wa kocha Mreno, Jose Mourinho.
    Tabasamu la neema; Adam Nditi mambo yanazidi kumnyookea Chelsea

    Lakini pia kutokana na kuonekana kukomaa kisoka, Nditi anaweza hata kutolewa kwa mkopo timu yoyote ya Ligi Kuu Ulaya ili akakusanye uzoefu wa kucheza na huo unaweza kuwa mwanzo wa kutimiza ndoto zake za kucheza Ligi kubwa za Ulaya.
    Nditi, aliyezaliwa Septemba 18, mwaka 1994 kisiwani Zanzibar, alianzia kikosi cha vijana chini ya umri wa miaka 13 Chelsea na ana uwezo wa kucheza beki au wingi ya kushoto. 
    Alichangia kwa kiasi kikubwa mafanikio ya timu ya akademi kutwaa Kombe la FA la Vijana mwaka 2012. 
    Mchezaji mkubwa; Ni jambo la kujivunia kufanya kazi na Mourinho, Nditi hapa anapata mafundisho ya Mreno huyo Chelsea wakati wa mazoezi ya kikosi cha kwanza

    Alikuwa mchezaji aliyecheza mechi nyingi zaidi za ligi na akacheza pia mechi nne za timu ya kikosi cha wachezaji wa akiba msimu wa 2011/2012, msimu wake wa kwanza baada ya kupata Mkataba rasmi wa mchezaji wa kulipwa Stamford Bridge.
    Akiwa akademi, alicheza mechi 27 pamoja na kuwa mchezaji wa kudumu katika Kombe la FA la Vijana mwaka 2011 ambako aliifikisha timu Nusu Fainali.
    Uchezaji wake wa kasi, akifuata nyayo za beki wa kimataifa wa England, Ashley Cole kiuchezaji, kwa kupanda akiwakimbiza wachezaji wa timu pinzani, umekuwa kivutio Chelsea.
    Kuanzia msimu wa 2012/2013 alipandishwa rasmi U-21, na kucheza mashindano yote, NextGen Series na Kombe la FA la Vijana.
    Kocha wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Mdenmark, Kim Poulsen alimuita Nditi mara kadhaa mwaka huu, lakini akashindwa kuja kujiunga na timu hiyo kwa sababu taratibu hazikufuata.
    Nditi amewahi kukaririwa akisema kwamba anaweza kuja kujiunga na Stars, iwapo TFF au kocha wa Stars atafuata taratibu za kumuombea ruhusa katika klabu yake na si kuitwa kupitia vyombo vya habari. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: NDITI MAMBO 'SUPA' CHELSEA, NDOTO ZA KUCHEZA LIGI KUBWA ULAYA KARIBU KUTIMIA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top