• HABARI MPYA

    Friday, October 04, 2013

    SIMBA SC NA WATOTO WA MKWASA KESHO TAIFA, AZAM NA COASTAL TANGA, YANGA SC NA MTIBWA

    Na Mahmoud Zubeiry, IMEWEKWA OKTOBA 4, 2013 SAA 1:16 ASUBUHI
    LIGI Kuu ya Vodacom Tanzania Bara inatarajiwa kuendelea kesho baada ya mapumziko ya wiki moja kuwapa ahueni kidogo wachezaji baada ya mechi nne ndani ya wiki mbili. 
    Vinara wa ligi hiyo, Simba SC wataendelea kubaki Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, wakihitimisha mechi zao dhidi ya timu za Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa kumenyana na Ruvu Shooting ya Pwani.
    Tayari Simba SC, inayofundishwa na mshambuliaji wake wa zamani, Alhaj Abdallah Athumani Seif ‘King Kibaden’ imekwishacheza na timu nyingine zote za JKT na kuzifunga zote, ambazo ni Oljoro ya Arusha (1-0), Mgambo ya Tanga (6-0) na JKT Ruvu (2-0).
    Ruvu Shooting inayofundishwa na kiungo wa zamani wa Yanga SC, Charles Boniface Mkwasa itajaribu kuzifuatia aibu timu nyingine za JKT kesho katika mchezo huo.
    Mkali wa mabao; Amisi Tambwe Kesho atakutana na George Michael

    Mshambuliaji mpya wa Simba SC, Amisi Tambwe  aliyevuna mabao saba katika mechi sita za awali za ligi hiyo za timu hiyo kesho atapigana kuongeza idadi ya mabao yake katika kuwania ufungaji bora wa Ligi Kuu.
    Hakuna shaka juu ya Tambwe ni mfungaji hodari akiwa tayari ana rekodi za kuchukua ‘kiatu cha dhahabu’ cha Ligi ya kwao Burundi na michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame.
    Lakini kesho Tambwe itabidi akabiliane na ubabe wa beki ‘mndava’ wa Ruvu Shooting, George Michael ili kuweza kuendeleza desturi yake ya kutikisa nyavu. George Michael kwa sasa ni miongoni mwa mabeki wanaogopewa katika Ligi Kuu na kesho itakuwa fursa ya Tambwe kudhihirisha umahiri wake mbele ya mlinzi huyo.  
    Mbali na mchezo huo, Uwanja wa Mkwakwani, Tanga, Azam FC watajaribu kusaka ushindi wa tatu msimu huu mbele ya wenyeji Coastal Union.
    Kocha Hemed Morocco wa Coastal amekwishaanza ‘kung’ong’wa’ kwamba timu imesajili wachezaji wazuri, lakini haifanyi vizuri kwa kuwa ameshindwa kuiunganisha vyema.
    Na kesho, Morocco atacheza dhidi ya timu ya bosi wake wa zamani katika timu ya taifa ya Zanzibar, Stewart Hall. Lakini Muingereza Hall pia anakabiliwa na changamoto ya matokeo mazuri, kwani hadi sasa katika mechi sita ameshinda mbili tu.
    Uwanja wa Azam Complex, JKT Ruvu wataikaribisha  Kagera Sugar, wakati Sheikh Amri Abeid mjini Arusha JKT Oljoro watakuwa wenyeji wa Mbeya City ambayo haijafungwa hata mechi moja, ingawa imecheza mara mbili ugenini hadi sasa.
    Ligi hiyo, inatarajiwa kuendelea keshokutwa, wakati mabingwa watetezi, Yanga SC watakapomenyana na Mtibwa Sugar Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na Uwanja wa Mkwakwani, Tanga Mgambo JKT wataikaribisha Prisons ya Mbeya.
    Hali si nzuri sana kwa mabingwa watetezi, Yanga SC kwani katika mechi sita wameshinda mbili, sare tatu na kufungwa moja- wakiwa wanazidiwa kwa pointi tano na Simba SC kileleni.
    George Michael kushoto akimpa konga Hamisi Kiiza wa Yanga, Tambwe anaye huyu leo

    Kocha Mholanzi, Ernie Brandts anaweza kugeuziwa kibao mara moja na kupewa tiketi ya kurejea kwao, iwapo Jumapili matokeo yatakuwa mabaya kwa wana Jangwani.
    Mwenyekiti wa Yanga SC, Yussuf Manji amekuwa karibu mno na timu siku za karibuni akifuatilia hadi mazoezi mbali ya kuhudhuria mechi kadhaa za timu hiyo- maana yake anajionea hali halisi.
    Alikuwepo wakati timu hiyo ikitoa sare ya 1-1 na Mbeya City mjini Mbeya na alikuwepo wakati timu hiyo ikipata ushindi mwembamba na wa jasho mbele ya Ruvu Shooting wiki iliyopita na katikati ya wiki akaibuka katika gym yake ya Quality Centre kuangalia wachezaji wakifanya mazoezi ya viungo.
    Wiki iliyopita wakitoka kufungwa na Azam FC 3-2, Manji alikutana kwa chakula cha usiku na wachezaji katika hoteli ya nyota tano, Hyatt Regency, zamani Kilimanjaro Kempinski na baada ya hapo timu ikapata ushindi wa kwanza ndani ya mechi tano wa 1-0 dhidi ya Ruvu Shooting.

    MSIMAMO WA LIGI KUU BARA

    TAN
    TAN
    RnkTeamMPWDLGFGA+/-Pts
    1 Simba SC64201541114
    2 Kagera Sugar632173411
    3 Azam624096310
    4 Coastal Union624063310
    5 Young Africans623111749
    6 JKT Ruvu63036429
    6 Ruvu Shooting63036429
    8 Mbeya City61506518
    9 Rhino Rangers714278-17
    10 Mtibwa Sugar614156-17
    11 JKT Oljoro612336-35
    12 Mgambo JKT6123210-85
    13 Tanzania Prisons604239-64
    14 Ashanti United7025415-112

    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: SIMBA SC NA WATOTO WA MKWASA KESHO TAIFA, AZAM NA COASTAL TANGA, YANGA SC NA MTIBWA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top