• HABARI MPYA

    Friday, January 17, 2014

    COASTAL WAWAWEKEA NADHIRI YANGA; LAZIME ‘WAFE’ MKWAKWANI

    Na Mahmoud Zubeiry, Muscat
    COASTAL Union ipo kambini hapa Oman kujiandaa na mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara na mechi ya pili itacheza na Yanga SC ya Dar es Salaam, ambayo ipo kambini pia Uturuki kujiandaa na hatua hiyo.
    Pamoja na kwamba wapinzani wao wako Ulaya, Mwenyekiti wa Coastal Union, Hemed Hilal ‘Aurora’ amesema kwamba Yanga wahesabu wamekwishafungwa katika mchezo huo wa pili wa Ligi Kuu mzunguko wa pili.
    Mabosi; Kutoka kulia Mwenyekiti wa Coastal, Hemed Hilala 'Aurora', Ofisa Ubalozi wa Tanzania nchini Oman, Said Mussa na Meneja wa Coastal, Akida Ahmed 'Machai' jana Uwanja wa Fanja timu hiyo kimenyana na wenyeji Fanja na kulala 1-0.

    Kipi kinawapa jeuri Coastal wakati wapinzani wao wapo Ulaya? “Sisi huku tunapata faida sana, kwa sababu tunacheza na timu za Ligi Kuu ya Oman ambazo nyingine zinacheza Ligi ya Mabingwa ya Asia,”alisema.
    Hata hivyo, Aurora amesema kwamba Yanga katika ziara yao Uturuki wanacheza na timu za madaraja ya chini na tena wanapangiwa wachezaji wa akiba na vikosi vya pili, hivyo hawapati ushindani wowote na hawana faida wanayopata, zaidi ya kwenda kutalii.
    “Wajipange sawasawa, wakija Tanga sisi tunawachapa, tena kisawasawa wafukuze tena kocha, maana wakifungwa wanavunja benchi la Ufundi,”alisema.
    Wakati Yanga itaanza na Ashanti United Uwanja wa Dar es Salaam, Coastal itafungua dimba na JKT Oljoro Uwanja wa Mkwakwani, Tanga kabla ya timu hizo kukutana katika mechi za pili za ligi hiyo.
    Mzunguko wa kwanza, Uwanja wa Taifa, Yanga ililazimishwa sare ya 1-1 na baada ya hapo mashabiki wake wakawafanyia vurugu wachezaji wa Coastal na kuvunja vioo vya basi lao.
    Yanga wapo Uturuki tangu Januari 9 na hadi sasa wamekwishacheza mechi tatu na kushinda zote, wakati Coastal katika mechi tatu wamefungwa moja na kushinda mbili tangu watue Oman Januari 9, mwaka huu. 
    Timu zote zinatarajiwa kurejea Tanzania Janauri 23, tayari kwa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu. Yanga ilimaliza Ligi mzunguko wa kwanza ikiwa kileleni kwa pointi zake 28 baada ya mechi 13, wakati Coastal ilimaliza katika nafasi ya nane kwa pointi zake 16. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: COASTAL WAWAWEKEA NADHIRI YANGA; LAZIME ‘WAFE’ MKWAKWANI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top