• HABARI MPYA

    Sunday, May 17, 2015

    MANJI NA KAMATI ZAKE YANGA SC, MATOKEO YAKE NDIYO HAYA YA KASWAHILI

    MEI 14, mwaka huu, yaani Alhamisi wiki hii, mtu aliyejitambulisha kama Katibu wa Kamati ya Uchaguzi ya Yanga SC, Francis Kaswahili alitoa tangazo la Uchaguzi Mkuu wa klabu hiyo, akisema utafanyika Julai 12, mwaka huu katika ukumbi ambao utatajwa baadaye.
    Taarifa ya Kaswahili iliyotumwa BIN ZUBEIRY na vyombo vingine vya habari siku hiyo, ilisema kwamba, fomu za wagombea zitaanza kutolewa Mei 17, mwaka huu kwa kuzingatia ratiba.
    “Jambo hili ni la kikatiba na wala halina mjadala, tunataka Yanga iwe na viongozi ambao watatokana na utashi wa Wanayanga ni matumaini ya kamati ya uchaguzi kwamba hapatatokea mtu mwingine wa kutaka kuvunja misingi ya katiba.
    “Huu ni utamaduni wa mwanadamu anayeishi katika mfumo wa demokrasia na hasa ikizingatiwa kwamba mwaka 2015 ni mwaka pia wa uchaguzi, wa Rais, Wabunge na Madiwani,”amesema Kaswahili. 
    Ameongeza kwamba, lengo ni mwendelezo wa kupokezana vijiti na kwamba kiongozi bora atapatikana kwa misingi bora ya kikatiba na si vinginevyo.
    Itakumbukwa kwamba kwa mara ya mwisho Yanga SC ilifanya uchaguzi wake Julai 18, mwaka 2010 na Wakili Lloyd Biharangu Nchunga alichaguliwa kuwa Mwenyekiti, Makamu wake, Devis Mosha na Wajumbe; Charles Mgondo, Ally Mayayi Tembele, Mzee Yussuf, Theonest Rutashobolwa (marehemu), Titus Ossoro, Sara Ramadhani, Mohamed Bhinda na Salum rupia. 
    Hata hivyo, kwa vipindi tofauti baadhi ya viongozi walijiuzulu nyadhifa zao na hivyo ikalazimika kufanyika uchaguzi mdogo ufanyike Julai 15, mwaka 2012 na Yussuf Manji alichaguliwa kuwa Mwenyekiti, Makamu wake Clement Sanga na Wajumbe; Aaron Nyanda, George Manyama, Abdallah Bin Kleb na Mussa Kutabaro. 
    “Na itakumbukwa kamba wale wote ambao waliingia kwa kuziba nafasi wazi walikuwa wanatumikia mhula ulioanza tarehe 18/07/2010 na ulikoma tarehe 17/07/2014 na hivyo viongozi wote nafasi zao kwa sasa zipo wazi,”alisema Kaswahili.
    Lakini jana, uongozi wa Yanga SC ukamkana Kaswahili na kumtishia pia kumshitaki kwenye Kamati ya Maadili ya TFF na Mahakamani.
    Akizungumza na Waandishi wa habari jana makao makuu ya klabu, Jangwani, Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Yanga, Dk. Jonas Tiboroha, amesema Mei 14 Kaswahili alitangaza uchaguzi na mchakato wake kinyume na katiba ya Yanga, kwa sababu yeye si kiongozi pia si mwanachama kwa sababu mara ya mwisho kulipa ada ni 2012.
    “Kisheria Kaswahili si mwanachama, kwani tangu 2012 hajalipa ada na kisheria usipolipa ada uanachama unakufa na unapaswa kuomba upya”, alisema Dk. Tiboroha.
    Alisema Yanga pia wanamshitaki kwa makosa ya kuchochea na kuharibu utulivu ndani ya klabu kwa kuitisha uchaguzi ikiwa ni batili na si kiongozi wa kamati ya uchaguzi wa Yanga.
    Kosa la pili ni kuidhalilisha klabu ya Yanga kwa kutumia jina lake kwa kujiita katibu wa kamati ya uchaguzi wa klabu wakati akijua dhahiri yeye si kiongozi katika kamati yoyote, pia si mwanachama hai wa Yanga.
    Tatu, ni kuongea mambo ya uongozi wa Yanga bila kuwasiliana na Sekretarieti ya Yanga na mwisho kutapeli wanachama wa Yanga kwa kutangaza bei ya fomu za uchaguzi bila maelekezo ya uongozi wa Yanga kuwa na taarifa.
    Tiboroha alisema Yanga ina uongozi uliochaguliwa kihalali wenye mamlaka kisheria na kikatiba kupanga na kutangaza mambo yake na si vinginenvyo, lakini pia akasikitishwa na baadhi ya vyombo vya habari kuandika habari ambayo haikukamilika.
    “Gazeti moja ambalo limeandika habari hizo tumeanza mchakato wa kulipeleka mahakamani na tunatafuta sauti zote zilizotangazwa na kila chombo cha habari ili kuvichukuliwa hatua za kisheria, kwani Yanga ipo wazi kuongea na waandishi aidha kwa kunipigia mimi simu au Jerry Muro ambaye ni Mkurungezi wa Mawasiliano wa klabu”, alisema Dk. Tiboroha.
    Aidha Tiboroha alisema walimuandikia Kaswahili barua juzi ya kumtaka kukanusha taarifa alizotangaza kupitia vyombo vya habari hadi jana saa sita mchana, lakini hakutekeleza ndiyo maana wameamua kumpeleka kwenye kamati ya maadili na kumfungulia mashitaka ya jinai na madai dhidi yake kwa gharama zake mwenyewe.

    KUHUSU FRANCIS KASWAHILI
    Huyu mtu kweli alikuwa katika Kamati ya uchaguzi iliyopita ya Yanga SC iliyomuweka madarakani, Mwenyekiti wa sasa Yussuf Manji.
    Lakini Kamati hiyo iliyokuwa chini ya Mwenyekiti, Jaji John Mkwawa, Makamu  Ridhiwani Kikwete, Katibu Kaswahili na Wajumbe Yusuph Mzimba na Philemon Ntahilaja ilivunjwa na Manji Machi mwaka jana.
    Manji akaunda Kamati mpya ya Uchaguzi chini ya Mwenyekiti Alex Mgongolwa, Makamu wake Jabir Katundu, Katibu Bakili Makele na Wajumbe Daniel Mlelwa na Mustafa Kajole.

    KAMATI MPYA KILA MARA ZINALETA MKANGANYIKO
    Yanga SC chini ya Manji mambo yanabadilika kila siku, watendaji wanaondolewa, wanakuja wapya na Kamati zenyewe kila mara zinabadilika.
    Manji baada ya Machi 14 kubomoa Kamati ya Uchaguzi, Julai mwaka jana akavunja Kamati zote hadi ya Utendaji na kuziunda upya.
    Mwishoni mwa Agosti pia mwaka jana, Manji akaunda Kamati mpya zenye Wajumbe kibao, kabla ya mwishoni mwa mwaka kubadilisha Sekretarieti nzima.
    Wazi katika mfumo wa mabadiliko ya mara kwa mara, inakuwa vigumu kwa vyombo vya habari wakati mwingine kutunza kumbukumbu.
    Na hapana shaka, Kaswahili ametumia mwanya huo kupenyeza taarifa zake potofu kwenye vyombo vya habari. 
    Lakini pia, taarifa ya Tiboroha inaonyesha walikuwa wanajua kitu alichokifanya Kaswahili kabla, nastaajabu kwa nini hawakutoa taarifa ya angalizo kwenye vyombo vya habari?
    Dk Tiboroha pia alisema walimuandikia Kaswahili barua juzi ya kumtaka kukanusha taarifa alizotangaza kupitia vyombo vya habari hadi juzi saa sita mchana, lakini hakutekeleza ndiyo maana wameamua kumpeleka kwenye kamati ya maadili na kumfungulia mashitaka ya jinai na madai.
    Kaswahili anastahili kuchukuliwa hatua za kinidhamu na kisheria Yanga SC kwa kitendo alichokifanya- ila tu tishio la kushitaki vyombo vya habari halina sababu.
    Dk Tiboroha, kiongozi msomi na mpya katika soka ya Tanzania, bila shaka atanielewa hapa, namna ambavyo vyombo vya vya habari vinakanganywa na mabadiliko ya Kamati za klabu hiyo mara kwa mara.
    Na mbaya zaidi, Kaswahili aliiandika kiufundi mno taarifa yake, kiasi kwamba si rahisi kuishitukia kama ni feki. 
    BIN ZUBEIRY, ikiwa moja ya vyombo vya habari vilivyochapisha taarifa ya Kaswahili, inaomba radhi kwa klabu na wanachama pamoja na wote waliokwazwa na taarifa hiyo.
    Hakuna sababu ya kuchukulia hatua vyombo vya Habari, bali na Yanga SC nayo iachane na mtindo wa kuunda Kamati mpya mara kwa mara, unakanganya. Alamsiki. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MANJI NA KAMATI ZAKE YANGA SC, MATOKEO YAKE NDIYO HAYA YA KASWAHILI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top