MASHABIKI wawili wenye hasira wamefungua kesi dhidi ya Manny Pacquiao kwa kushindwa kuandika ana maumivu ya bega katika fomu maalum ya taarifa za bondia kabla ya pambano lake na Floyd Mayweather alilopoteza kwa pointi Alfajiri ya Mei 3.
Mfilipino huyo mwenye umri wa miaka 36 anaweza kuwa nje ya ulingo hadi mwaka wakati akijiandaa kwenda kufanyiwa upasuaji wa bega, maumivu ambayo hakusema kabla ya pambano lililofanyika ukumbi wa MGM Grand mjini Las Vegas, Marekani.
Taarifa ya ESPN imesema wakazi wa Nevada, Stephane Vanel na Kami Rahbaran wanamshitaki bondia huyo kwa niaba ya watu wote walionunua tiketi kwenda kushuhudia pambano hilo, kulipia kuona kwenye televisheni au walioweka 'madau'.
BIN ZUBEIRY imeipata nakala ya fomu ya maelezo muhimu ya bondia kabla ya pambano, ambayo inaonyesha kwamba Pacquiao alitumia dawa kadhaa za maumivu.
Aidha, neno hapa likiwa linafuatia limepigiwa mstari baada ya swali; ‘Ulikuwa una maumivu yoyote kwenye mabega yako, chini ya mabega, au mikononi ambayo yanahitaji vipimo vya uthibitisho wa kupona?’
Kwa kusaini fomu hiyo, wote Pacquiao na mshauri wake Michael Koncz wanaweza kuchukuliwa hatua kwa sababu, mwishoni kuna maelezo yasemamo; "Maelezo ya hapo juu ni kweli na sahihi nikiwa na akili zangu timamu,".
Adhabu ya kosa hilo kwa kawaida huwa ni kufungwa jela kati ya mwaka mmoja na minne na kutozwa faini hadi dola za Kimarekani 5,000 (Sh. Milioni 20). Pacquiao anaweza pia kutozwa faini na kufungiwa na Kamisheni ya Michezo Nevada.
Mwenyekiti wa Kamisheni, Francisco Aguilar amesema kwamba ofisi ya Mwanasheria Mkuu itachunguza kwa nini maumivu hayo hayakuorodheshwa.
"Na tutafanya majadiliano fulani. Kwa sababu Kamisheni inapaswa kupata maelezo ya kila wakati ya bondia. Tiba aliyopata iliorodheshwa kwenye fomu, lakini si ya maumivu halisi. Hili si pambano letu la kwanza. Hii ni biashara yetu. Kuna utaratibu, na unapojaribu kukiuka utaratibu, hatuwezi kufanya kazi na wewe,"amesema.
Floyd Mayweather alipigana kwa ustadi wa hali ya juu dhidi ya mpinzani wake huyo mjini Las Vegas
0 comments:
Post a Comment