• HABARI MPYA

    Saturday, June 09, 2012

    POULSEN AWALALAMIKIA TFF KUTOMPATIA DVD ZA GAMBIA


    Poulsen akizungumza na Waandishi wa Habari ofisi za TFF leo asubuhi

    KOCHA wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Kim Poulsen amesikitishwa na kitendo cha Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kushindwa kumpatia DVD za mechi za Gambia kuelekea mechi ya kesho ya Kundi C, baina ya timu hizo kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Dunia 2014.
    Akizungumza na Waandishi wa Habari katika ofisi za TFF leo, Mdenmark huyo amesema hii ni mara ya pili anaomba DVD, lakini anashindwa kupatiwa, kwani awali aliomba DVD za Ivory Coast kabla ya mechi ya Jumamosi iliyopita mjini Abidjan, ambayo Stars ilifungwa 2-0.
    Pamoja na kukosa DVD hizo, lakini Poulsen amesema amewaandaa vizuri vijana wake kwa ajili ya mechi ya kesho, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Poulsen alisema kambi yake inaendelea vizuri na anafurahi kiungo mshambuliaji Haruna Moshi Shaaban ‘Boban’ anaendelea vizuri na anaweza akacheza kesho.
    Hata hivyo, katika Mkutano huo ambao ulikuwa maalum kwa makocha wote akiwemo wa Gambia, kuzungumzia mchezo huo, lakini wageni hawakutokea kabisa.
    Hata hivyo, jana BIN ZUBEIRY ilizungumza na kocha Mkuu wa Nge wa Gambia, Mtaliano, Luciano Machini ambaye alisema mechi ya Jumapili itakuwa ngumu kwa sababu wapinzani wao ni wazuri.
    Akizungumza na BIN ZUBEIRY katika mazoezi ya timu hiyo jioni ya jana Uwanja wa karume, Machini aliyechukua nafasi ya aliyekuwa bosi wake, Peter Bonu Johnson, Mei mwaka huu, amesema kwamba Taifa Stars ni wazuri na wana kasi uwanjani, hivyo mechi hiyo hata wachezaji wake wanajua itakuwa ngumu.
    Alisema wao walicheza vizuri dhidi ya Morocco kwenye mechi yao ya kwanza, lakini wanaingia kwenye mechi ngumu na wenyeji Jumamosi.
    Kocha Machini na BIN ZUBEIRY
    Machini aliwaongoza vijana wake kwa mazoezi mepesi jioni ya leo Uwanja wa Karume na inaonekana kama ana majeruhi wasiopungua watatu, ingawa benchi la ufundi la timu hiyo kwa ujumla limefanya siri juu ya hali za afya za wachezaji wao.
    Nge wa Gambia waliotoka sare ya 1-1 nyumbani na Morocco kwenye mechi ya kwanza Jumamosi, waliwasili nchini jana saa 5.30 usiku kwa ndege ya Kenya Airways tayari kwa mechi dhidi ya Taifa Stars, iliyofungwa 2-0 na Ivory Coast katika mechi ya kwanza ya Kundi hilo Jumamosi mjini Abidjan, itakayochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Msafara wa timu hiyo wenye watu 31 wakiwemo wachezaji 22 unaongozwa na
    Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Vijana na Michezo wan chi hiyo, Malang Jassey.
    Viongozi wengine ni Ofisa Utawala wa timu Modou Sowe, Kocha Luciano Machini, makocha wasaidizi Peter Bonu Johnson na Lamin Sambou, Kocha wa makipa Alhagie Marong, mtaalamu wa tiba mbadala (physiotherapist) Pa Matarr Ndow, Mtunza vifaa Sanna Bojang na Daktari wa timu Kalifa Manneh.
    Wachezaji ni Musa Camara, Abdou Jammeh, Momodou Futty Danso, Lamin Basmen Samateh, Ousman Koli, Pa Saikou Kujabi, Mustapha Kebba Jarju, Yankuba Mal Ceesay, Demba Savage, Saihou Gassama, Alieu Darboe, Momodou Ceesay, Pa Modou Jagne, Tijan Jaiteh, Bubacarr Sanyang, Christopher Allen, Musa Yaffa, Sulayman Marr, Mamut Saine, Hamsa Barry, Ali Sowe, Omar Colley na Saloum Faal.
    Baada ya mazoezi ya leo, Nge hao, watafanya tena mazoezi yao kesho asubuhi Uwanja wa Karume na jioni Uwanja wa Taifa. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: POULSEN AWALALAMIKIA TFF KUTOMPATIA DVD ZA GAMBIA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top