• HABARI MPYA

    Sunday, June 03, 2012

    TUKIWAWEKA KWENYE MIZANI TENGA, NDOLANGA, TENGA...


    Na Mahmoud Zubeiry

    KATIKA Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) mwaka huu- jambo ambalo naweza kuliita kubwa lilikuwa ni kuteuliwa kwa Said Hamad El Maamry na Muhiddin Ahmad Ndolanga kuwa marais wa heshima wa shirikisho hilo.
    Wawili hawa, wote ni viongozi wa zamani wa juu wa soka ya Tanzania, ambao viongozi waliowafuatia wameshindwa kuvunja rekodi zao hadi sasa.
    El Maamry, wakati wake soka ilikuwa ina heshima, hadhi na mafanikio na ni wakati wake ndipo Tanzania ilicheza Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 1980 nchini Nigeria.
    Jambo moja tu, ambalo wachezaji wa zamani wamekuwa ‘wakimlaani’ El Maamry alibana mno wachezaji wa Tanzania kucheza nje na pia katika hilo inawezekana walikuwa wanamuonea, pengine ilitokana na sera za nchi wakati huo, ambazo yeye labda alishindwa kupambana nazo.
    Ndolanga, alikuwa ana wakati mgumu sana katika utawala wake, pamoja na kwamba alijitahidi kupambana na chuki na vita dhidi yake na wakati huo huo alifanya jitihada za kupanga mikakati na kutekeleza mipango ya maendeleo ya soka ya Tanzania.
    Alhaj Ndolanga wakati wake walimuita Tyson, eti wakimuona ni mbabe kutokana na misimamo yake- lakini leo ukitazama hali halisi enzi zake, unagundua babu alitolewa ‘kafara’ tu.
    Mambo yasiyopungua matatu yalimkwamisha Ndolanga katika utawala wake, katiba mbovu iliyotoa fursa ya migogoro na mapinduzi, pili timu au watu aliokuwa akifanya nao kazi kuwa aidha wasaliti au watu wenye upeo mdogo na wasio waadilifu na tatu ni Profesa Juma Athumani Kapuya, ambaye alikuwa anamuingilia mno na kuonekana dhahiri anampiga vita wakati akiwa Waziri anayehusika na michezo.
    Madudu mangapi yalifanywa na Kapuya akiwa Wizara ya michezo tena ya kihistoria, lakini nitakumbushia machache tu. Kuingilia mfumo wa Ligi Kuu kwa kuongeza timu kinyume na makubaliano kati ya FAT na waliokuwa wadhamini, Bia ya Safari Lager hadi wakaamua kujitoa mwaka 2001 na kusababisha timu zikose fedha za udhamini, ikiwemo zawadi za washindi mbalimbali hadi bingwa wa mwaka huo, Simba SC.
    Kuingilia na kuvuruga usajili, kuamua bingwa mezani mwaka 1999, wakati Yanga tayari imetwaa taji kwa matokeo ya uwanjani, akapitia rufaa na kutoka matokeo, akawapa ubingwa Mtibwa Sugar. Jamani ni mengi na hatujasahau, kwani kiasi kikubwa miaka 10 ya Kapuya kuwa kwenye wizara yenye dhamana ya michezo, ilikuwa kikwazo kikubwa cha maendeleo ya mchezo huu na mingine mingi nchini.
    Alishindwa kuondoka amri ya kuzuia michezo mashuleni, akiwa Waziri mwenye dhamana ya michezo- hakujua kama wanamichezo wazuri huanzia kutengenezwa wangali wadogo mashuleni. Aliona poa tu. Kapuya huyo! Profesa.
    Pamoja na yote, Ndolanga alionyesha uhodari wake kwa kuendelea kuongoza soka ya nchi hii licha ya hali ngumu pia ya kiuchumi wakati huo, kutokana na wadau, makampuni kutosaidia mchezo huo, kwa kuamini umegubikwa na fujo na migogoro.
    Timu ya taifa haikuwa na wadhamini, alijaribu kuwahusisha wafanyabiashara wakubwa kama Reginald Mengi, Azim Dewji, Mohamed Dewji na wengineo kusaidia timu. Tulishiriki mashindano karibu yote, kuanzia ya vijana, wanawake na wakubwa.
    Msisimko wa soka ya Tanzania enzi za utawala wa Ndolanga ni tofauti mno na ligi laini laini tunayoiona leo. Kama yapo mabaya ya Ndolanga aliyeanza kuongoza soka ya nchi hii mwaka 1991 katika kamati ya Muda, kabla ya kuchaguliwa rasmi 1993 kwa kura na kudumu hadi 2004, alipoangushwa na Leodegar Chilla Tenga, hakuna hakika kwenye mizani yatazidi mazuri yake.
    Fursa ambayo ameipata Tenga ya kuungwa mkono na wadau, makampuni, wafadhili, serikali na kulindwa na katiba mpya iliyotokana na mwongozo wa FIFA, Uwanja mpya wa Taifa hapana shaka na Ndolanga angevipata, leo tungekuwa tunazungumza lugha tofauti kuhusu yeye.
    Si wakati wa kuoneana haya tena, zaidi ya kuambiana ukweli kwa manufaa ya soka yetu. Sijali, atakayenichukia, kunitenga shauri yake, lakini daima nitasimamia katika ukweli na hiyo kwa sababu ya uzalendo wangu na mapenzi yangu katika soka. Miaka nane ya Tenga kuwapo madarakani, imetosha kujua uwezo wake na kwa kumlinganisha na Ndolanga, jibu lipo wazi. Kipindi kigumu alichopitia Ndolanga, na hali halisi ya soka yetu ilivyokuwa kama nilivyoelezea hapo juu, kulinganisha na mambo yalivyo sasa, inamaanisha babu alikuwa ‘babu kubwa’.
    Tanzania aliyoiongoza Mwalimu Julius Kabarage Nyerere, si Tanzania anayoiongoza Jakaya Mrisho Kikwete leo. Tanzania ya leo ni nzuri na changamoto kubwa inayowakabili wakuu wa nchi ni kupanuka kwa demokrasia na uhuru wa maoni, lakini nchi ile aliyoiongoza Mwalimu, hakuna hakika kama Jakaya, Benjamin William Mkapa au Ally Hassan Mwinyi wangeiweza. Vivyo hivyo, mazingira aliyofanyia kazi Ndolanga katika soka ya nchi hii, dhahiri Tenga asingeweza. Tena kabisa.
    Pamoja na mengi ambayo tunaamini yalikuwa mazuri kutoka kwa Ndolanga, kubwa lililokuwa linavutia wengi ni jinsi alivyowathamini makocha wazawa, kuwapa fursa za kujiendeleza kielimu na kuwapa majukumu ya kufanya kazi katika timu za taifa.
    Tangu mwaka 1991 hadi 2004, Ndolanga ameacha hazina kubwa ya makocha wazawa wa kiwango cha kimataifa ambao ndio leo TFF ya Tenga inawatumia kama ‘madeiwaka’ akina Charles Boniface Mkwasa na Sylvester Marsh. Labda watu watakuwa hawajui kuhusu Marsh, huyu jamaa alikuwa anafundisha watoto Mwanza, Ndolanga alimuona huko akamchukua na kumuendeleza kabla ya kumpa majukumu ya kufundisha timu za taifa za vijana.
    Hata lilipokuja shinikizo la kuleta kocha wa kigeni, bado imani ya Ndolanga ilibaki kwa makocha wazawa- kwa mfano mwaka 2002 kulikuwa kuna kocha Mjerumani Burkhad Pape, ila baada ya miaka miwili ya kuwapo kwake nchini kama kocha mkuu wa timu ya taifa bila mafaniko yoyote, akaamua kumfanya Mkurugenzi wa Ufundi na Syllersaid Salmin Kahema Mziray (sasa marehemu) pamoja na Charles Boniface Mkwasa wakapewa jukumu la ukocha wa timu ya taifa.
    Kwa mabadiliko hayo, Tanzania ikatwaa Kombe la kwanza lenye hadhi ya Afrika, CECAFA Castle Cup, mwaka 2002 michuano iliyokuwa inashirikisha  timu za taifa za Afrika Kusini, DRC, Ghana na jirini zetu Kenya na Uganda. Mwaka huo huo, Tanzania ikafika fainali ya Kombe la Challenge kwa mara ya kwanza baada ya miaka sita na kufungwa na Kenya 3-2 na Kenya mjini Mwanza.
    Kenya iliyoifunga Tanzania ilikuwa ina kikosi kikali haswa, ambacho miaka miwili baadaye ilifuzu kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika nchini Tunisia, kikiundwa na wakali kama Mussa Otieno, Dennis Oliech, John Oliech, Titus Mulama, Geoffrey Mangenge ‘Osama’ na wengineo.
    Tulizikosa kosa kidogo tu fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika 1996 nchini Burkina Faso, kama si kufungwa mechi ya mwisho na Algeria Julai 30, mwaka 1995 mjini Algiers mabao 2-1, siku hiyo Nahodha wetu Stars enzi hizo, Hussein Amaan Marsha akiwafungia bao la kusawazisha wapinzani dakika ya 29, baada ya Mohamed Hussein Daima ‘Mmachinga’ kuifungia Tanzania bao la kuongoza dakika ya 21, kabla ya Amrouche kutupiga bao la pili dakika ya 59 na kuipa Algeria tiketi ya kwenda Burkina Faso, ikiungana na vinara wa kundi letu, Misri.
    Misri ilimaliza na pointi 15, Algeria waliokuwa wa pili pointi 13, Uganda waliokuwa wa tatu walimaliza na pointi 10, wakati sisi (Tanzania) katika nafasi ya nne tulimaliza na pointi nane. Ila kama tungewafunga Algeria, wangebaki na pointi zao 10, hivyo tungefikisha pointi 11 na kuwa wa pili na kufuzu kwenye fainali hizo.
    Pamoja na kwamba kwenye kampeni hizi kocha Mbrazil Clovis de Oliviera alihusika, lakini bado kulikuwa kuna mchango mkubwa wa makocha wazalendo akina Mzee Heri na Kayuni. Hakika kwa hili makocha wazawa watamkumbuka sana Ndolanga, ambaye kwa sasa yupo nje ya ulingo wa soka, baada ya kuangushwa kwenye uchaguzi mwaka 2004. Na kwa sababu hiyo, leo nawapongeza TFF, hawakukosea kuwapa heshima hiyo El Maamry na Ndolanga. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: TUKIWAWEKA KWENYE MIZANI TENGA, NDOLANGA, TENGA... Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top