• HABARI MPYA

    Thursday, December 12, 2013

    BINGWA MPYA CHALLENGE APATIKANA LEO, STARS NA ZAMBIA BONGE LA MECHI NYAYO

    Na Mahmoud Zubeiry, Nairobi
    BINGWA mpya wa Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Challenge 2013 anatarajiwa kupatikana leo jioni wakati wa Fainali itakayozikutanisha Sudan ‘Mwewe wa Jangwani’ dhidi ya wenyeji, Kenya ‘Harambee Stars’
    Mchezo huo utatanguliwa na mechi mbili, kwanza ya wakongwe waliowahi kung’ara na Kenya enzi hizo ‘Wazee wa Kazi’ dhidi ya Tanzania ‘All Stars’ utakaochezwa Uwanja wa City, kuanzi Saa 7:00 mchana na baadaye mchezo wa kusaka mshindi wa tatu kati ya Zambia ‘Chipolopolo’ na Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars’ Saa 8:00 mchana Uwanja wa  Nyayo.
    Taji la sita katika miaka 50 ya Uhuru?; Kenya leo inamenyana na Sudan katika fainali ya Challenge Uwanja wa Nyayo, Nairobi

    ORODHA YA MABINGWA;

    1973  Uganda      
    1974  Tanzania    
    1975  Kenya       
    1976   Uganda      
    1977  Uganda      
    1978  Malawi      
    1979  Malawi      
    1980  Sudan       
    1981  Kenya       
    1982  Kenya       
    1983  Kenya       
    1984  Zambia      
    1985  Zimbabwe 
    1986   Haikufanyika
    1987  Ethiopia    
    1988  Malawi      
    1989  Uganda      
    1990  Uganda      
    1991  Zambia      
    1992  Uganda      
    1993   Haikufanyika 
    1994  Tanzania    
    1995  Zanzibar    
    1996  Uganda      
    1997   Haikufanyika 
    1998   Haikufanyika 
    1999  Rwanda B 
    2000  Uganda      
    2001  Ethiopia    
    2002  Kenya       
    2003  Uganda      
    2004  Ethiopia    
    2005  Ethiopia    
    2006  Zambia      
    2007  Sudan       
    2009  Uganda      
    2009  Uganda      
    2010  Tanzania
    2011  Uganda
    2012  Uganda
    2013   ???????
    Waliokuwa mabingwa watetezi, Uganda ‘The Cranes’ walivuliwa taji hilo na Kilimanjaro Stars baada ya kutolewa katika Robo Fainali mjini Mombasa kwa mikwaju ya penalti 3-2 kufuatia sare ya 2-2 ndani ya dakika 90.  
    Kenya iliifunga Tanzania Bara 1-0 kwa mbinde katika Nusu Fainali, wakati Sudan iliitoa Zambia kwa mabao 2-1.
    Harambee Stars, ambayo imewahi kushiriki mara tano fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika, ingawa haijawahi kuingia raundi ya pili zaidi ya kunusa na kutolewa imepania kutwaa taji leo, nchi yake ikisherehekea miaka 50 ya Uhuru. 
    Kenya walioshiriki fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mara nne, katika miaka ya 1988, 1990, 1992 na 2004 na mara zote wakitolewa raundi ya kwanza, ni mabingwa mara tano wa Kombe la Challenge la CECAFA katika miaka ya 1975, 1981, 1982, 1983 na 2002, hivyo leo itakuwa inawania taji la sita.
    Sudan inayojulikana kwa jina la utani kama Sokoor Al-Jediane Kiarabu, Kiingereza Desert Hawks, yaani Mwewe wa Jangwani, leo itakuwa inawania taji la nne la Challenge baada ya awali kulitwaa katika miaka ya 1980, 2006 na 2007 na wamekuwa wa pili mara mbili 1990 na 1996 na washindi wa tatu mara mbili pia, 1996 na 2004.
    Sudan ilikuwa moja ya nchi tatu tu nyingine zikiwa ni Misri na Ethiopia zilizoasisi Kombe la Mataifa Huru ya Afrika mwaka 1957 na ilifanikiwa kushinda taji hilo mwaka 1970, wakiwa wenyeji, baada ya kuwafunga Ghana 1-0 kwenye fainali, wakitoka kuifunga Misri 2-1 katika Nusu Fainali. 
    Sudan ni miongoni mwa timu kongwe barani Afrika na ilikuwa ina historia ya utajiri wa soka miaka ya 1950 na 1970, ambayo iliwahi kushika nafasi ya pili kwenye michuano hiyo katika fainali za mwaka 1959 zilizofanyika mjini Cairo, Misri zikishirikisha nchi tatu, yani mbali na wenyeji, pia walikuwapo Ethiopia. Ilishika tena nafasi ya pili katika fainali za mwaka 1963 baada ya kufungwa na Ghana 3-0 kwenye fainali, wakati 1957 ilikuwa ya tatu. 
    Stars itamenyana na Zambia (chini) kusaka mshindi wa tatu

    Mkali wa mabao wa sasa wa Challenge, Salah Ibrahim ndiye tegemeo la Mwewe wa Jangwani katika kampeni za taji la nne la michuano hiyo leo, wakati Harambee itamtegemea Alan Wanga.
    Mechi za leo zote zinatarajiwa kuwa nzuri, kutokana na ukweli kwamba timu zote ni bora. Bingwa wa michuano hiyo, anatarajiwa kupewa kitita cha dola za Kimarekani 30,000, mshindi wa pili dola 20,000 na wa tatu dola 10,000.  
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: BINGWA MPYA CHALLENGE APATIKANA LEO, STARS NA ZAMBIA BONGE LA MECHI NYAYO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top