Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Poppe kushoto akimkabidhi jezi ya Simba Daniel Akuffo baada ya kusajiliwa. Katikati ni Makamu Mwenyekiti wa Simba SC, Geoffrey Nyange 'Kaburu' |
Na Mahmoud Zubeiry
SIMBA SC imesema kwamba hakuna ‘ufisadi’ wa aina yoyote
katika zoezi la usajili katika klabu hiyo kutokana na utaratibu mzuri uliowekwa
na mshambuliaji Danny Mrwanda aliachwa kwa sababu ya dau kubwa alilotaka.
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Poppe
amekanusha kwa nguvu zote madai kwamba wachezaji huombwa ‘twenty percent’ ili
kusajiliwa na kusistiza kwamba Mrwanda alishindana na klabu hiyo ndiyo maana
akaachwa.
“Alitaka dau kubwa, baadaye akakubali dau tulilotaka kumpa,
baadaye tena ajaka anatutajia timu nyingine inamtaka, sisi tukamuambia basi
nenda kwenye hiyo timu nyingine, ndivyo tulivyoachana naye huyo bwana,”alisema Hans
Poppe.
Mrwanda alijiunga tena na Simba na Juni mwaka huu, akitokea
Vietnam alipokuwa anacheza soka ya kulipwa, lakini baada ya michuano ya Klabu
Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, Julai mwaka huu akatemwa.
Baada ya kutemwa Mrwanda, akasajiliwa mshambuliaji Daniel
Akuffo kutoka Ghana ambaye hata hivyo, kocha Mserbia Milovan Cirkovick haridhishwi
na uwezo wake.
Mrwanda aliwahi kumzungumzia Akuffo na kusema tatizo ni
twenty percent, jambo ambalo sasa Hans Poppe anakanusha.