• HABARI MPYA

    Wednesday, December 11, 2013

    ALHAJ NDOLANDA TYSON ‘AMTEMA MATE’ KIM POULSEN, ASEMA SI KOCHA NI MBABAISHAJI NA HATAIFIKISHA POPOTE STARS

    Na Asha Kigundula, Nairobi
    MWENYEKITI wa zamani wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF, tangu ikiitwa FAT, yaani Chama cha Soka Tanzania), Alhaj Muhiddin Ahmed Ndolanga 'Tyson' amesema kwamba hakuna sababu ya Kim Poulsen kuendelea kufundisha timu ya taifa, Taifa Stars kwa kuwa ameonyesha ni mbabaishaji na hana uwezo wa kulieletea taifa mafanikio.
    Akizungumza mara baada ya mchezo wa Nusu Fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Challenge kati ya Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars na wenyeji, Kenya ‘Harambee Stars’ jana Uwanja wa Nyayo, Nairobi mjini hapa, Ndolanga alisema Poulsen kwamba Kim ni ‘bure’.
    Kim mbabaishaji; Alhaj Muhiddin Ndolanga amesema Kim Poulsen hataifikisha popote Tanzania

    Ndolanga alisema baada ya Kenya kutangulia kupata bao, dakika ya nne, waliiachia Kili Stars nafasi ya kucheza mpira kwa dakika zote 86 zilizobaki, lakini ikashindwa kusawazisha bao hilo.
    Ameshauri TFF kuangalia upya suala la kocha, kwani tayari Kim raia wa Denmark, ameonekana kushindwa kuiletea Tanzania mafanikio.
    "Haiwezekani kocha ashindwe kutuletea ushindi katika dakika 86,”alisema Ndolanga na kuongeza kwamba Kili Stars ni timu nzuri, lakini tatizo ni benchi la Ufundi, chini ya kocha huyo Mdenmark, ambaye hana maamuzi ya haraka pale anapoona mipango yake imekwama.
    Ndolanga ni Mjumbe wa heshima wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) na yupo nchini hapa kama moja ya Makamisaa wa mechi za Challenge.
    Mbabaishaji? Poulsen ameitwa mbabaishaji na Alhaj Ndolanga
    Kilimanjaro Stars jana ilifungwa 1-0 na Harambee Stars katika Nusu Fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Challenge Uwanja wa Nyayo, Nairobi, usiku huu, bao pekee la mshambuliaji wa Thika United, Clifton Miheso dakika ya nne.
    Kwa matokeo hayo, sasa Stars itamenyana na Zambia katika mechi ya kusaka mshindi wa tatu kesho mchana Uwanja wa Nyayo tena, wakati Kenya itamenyana na Sudan katika Fainali jioni yake.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: ALHAJ NDOLANDA TYSON ‘AMTEMA MATE’ KIM POULSEN, ASEMA SI KOCHA NI MBABAISHAJI NA HATAIFIKISHA POPOTE STARS Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top