• HABARI MPYA

    Sunday, June 08, 2014

    WANACHAMA YANGA SC WAMSHITAKI MANJI TFF

    Na Samira Said, DAR ES SALAAM
    BAADHI ya wanachama wa Klabu ya Yanga wamemuandikia barua Rais wa Shirikisho la Soka Nchini (TFF), Jamal Malinzi, wakimtaka awasaidie kuitisha Uchaguzi Mkuu wa klabu hiyo kwa sababu viongozi waliokuwepo madarakani chini ya Mwenyekiti, Yussuf Manji wamemaliza muda wao kwa mujibu wa katiba.
    Akizungumza leo mjini Dar es Salaam, mmoja wa wanachama wa Yanga, Juma Magoma (2319) alisema kuwa wanamuomba Malinzi aitishe uchaguzi wa Yanga ndani ya siku 90 na endapo asipofanya hivyo, katiba ya klabu hiyo itaendelea kuvunjwa.
    Mwenyekiti wa Yanga SC, Yussuf Manji kulia akiwa na Makamu wake, Clement Sanga

    Magoma alisema wao wanatofautiana na maamuzi yaliyopitishwa katika mkutano mkuu uliofanyika Juni Mosi mwaka huu kwamba uchaguzi wa klabu hiyo ufanyike Juni 15 mwakani.
    Mwanachama huyo alisema kuwa kuruhusu viongozi waliopo kuendelea kuwaongoza ni kudhihirisha wazi wote hawaifahamu katiba ya Yanga, TFF na Baraza la Michezo la Taifa (BMT).
    "Tunamuomba Rais (Malinzi) atutangazie uchaguzi Yanga ndani ya siku 90 na kama (alitaja jina la kiongozi) anahitaji kukaa madarakani mwaka mmoja basi agombee tutampa kura, halafu ajiuzulu na si kwa kufanya anavyotaka yeye," alisema Magoma.
    Naye Goefrey Mwaipopo (2481) alisema kuwa katika klabu yao kuna mkanganyiko wa katiba na kueleza kwamba katiba iliyopo kwa Kabidhi Wasihi (Msajili wa Klabu na Vyama vya Michezo) ni ya mwaka 1968 na ndiyo inayolipiwa.
    Mwaipopo alisema pia bado katika nyaraka za kisheria, mdhamini anayetambulika ni Ramadhan Mwinyi Kambi na si Mama Fatma Karume kama inavyojulikana sasa.
    " Ramadhan Mwinyi Kambi naye ni mzee sana kwa sasa na alimkabidhi kisheria Juma Mwambelo, awe mdhamini wa klabu, sio Fatma Karume," alieleza Mwaipopo.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: WANACHAMA YANGA SC WAMSHITAKI MANJI TFF Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top