• HABARI MPYA

    Wednesday, December 11, 2013

    HAKUNA ZAWADI ZA FEDHA TASLIMU CHALLENGE YA MWAKA HUU, YOTE KAYATAKA CANNAVARO

    Na Mahmoud Zubeiry, Nairobi
    BARAZA la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), limesema kwamba safari hii halitatoa fedha taslimu za zawadi kwa washindi wa michuano ya Kombe la CECAFA Challenge na badala yake watatuma fedha moja kwa moja kwenye akaunti za Mashirikisho ya Soka za nchi husika.
    Katibu wa CECAFA, Nicholaus Musonye amewaambia Waandishi wa Habari katika Mkutano uliofanyika kwenye hoteli ya Hill Pack, Nairobi leo mchana kwamba wameamua kutumia mfumo wa kisasa ili kuepuka matatizo mbalimbali na pia kuzingatia usalama wa fedha zaidi.
    Katibu wa CECAFA, Nicholaus Musonye katikati akizungumza na Waandishi wa Habari leo mchana. Kulia ni Katibu wa FKF, Michael Esakwa na kushoto Makamu wa Rais, Eobert Asembo 

    “Safari hii hatutoa fedha uwanjani, tutakabidhi mfano wa hundi na mataji kwa washindi, baada ya hapo fedha zitatumwa kwenye akaunti zao,”alisema.
    Moja ya sababu za kufanya hivyo Musonye amesema ni kuepuka matatizo kama yaliyojitokeza mwaka jana mjini Kampala, Uganda baada ya washindi wa tatu Zanzibar kukabidhiwa zawadi zao.
    Aliyekuwa Nahodha wa Zanzibar, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ baada  ya kupokea fedha hizo, alikwenda kugawana na wachezaji wenzake badala ya kuziwasilisha kwa uongozi.
    Baadaye Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) kikaagiza wachezaji wote warejeshe fedha hizo, lakini baadhi akiwemo Cannavaro wa Yanga SC na Aggrey Morris wa Azam wakagoma jambo ambalo limesababisha wafungiwe kuchezea timu ya taifa kwa muda usiojulikana.
    Babu umeharibu; Nadir Haroub 'Cannavaro' amefanya CECAFA isitoe 'keshi' zawadi za washindi Challenge

    Bingwa wa CECAFA Challenge ataendelea kupata dola za Kimarekani, 30,000 mshindi wa pili 20,000 na wa tatu 10,000.
    Aidha, Musonye alisema maandalizi yote kuelekea Fainali ya CECAFA Challenge mwaka huu yamekamilka na mechi zitachezwa Uwanja wa Nyayo kuanzia saa 8:00 mchana mshindi wa tatu kati ya Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars’ na Zambia Chipolopolo na baadaye Fainali kati ya Kenya na Sudan.
    Aidha, Musonye alisema kutakuwa pia na mechi ya wachezaji wa zamani wa Kenya, Wazee wa Kazi dhidi ya Tanzania Bara ‘Tanzania All Stars’ ambayo itachezwa Uwanja wa City, Nairobi kuanzia Saa 7:00 mchana.  
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: HAKUNA ZAWADI ZA FEDHA TASLIMU CHALLENGE YA MWAKA HUU, YOTE KAYATAKA CANNAVARO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top