Kulia Samatta akishangilia bao lake alilofunga jana
MSHAMBULIAJI chipukizi wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta ameanza msimu mpya vizuri katika klabu yake, Tout Puissant Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Jana Ijumaa, TP Mazembe iliikung’uta 5-0 Tshinkunku kwenye Uwanja wa Frederic Kibassa Maliba mjini Lubumbashi na Samatta aling’ara na kufunga bao moja.
Mshambuliaji huyo wa zamani wa African Lyon na Simba ndiye aliyekata utepe hiyo juzi akifunga bao dakika ya 15 kabla ya Tressor Mputu kufunga la pili dakika ya 18 na la nne dakika ya 42, wakati Tusilu alifunga la tatu dakika ya 21 na Tshilembi akapiga la nne dakika ya 34.
Kipa wa Mazembe Robert Kidiaba alikuwa burudani baada ya kuingia uwanjani na kuanza kusoma biblia kabla ya mechi kuanza.
Katika mchezo huo, kikosi cha Mazembe kilikuwa; Kidiaba, Ndonga, Kimwaki, Mwepu, Kasusula, Ilongo, Tusilu/Lusadisu dk 74, Partcik Ochan, Mbwana Samatta/Salakiaku dk 82, Mputu, Lungu/Kanda dk 64.
Wakati Samatta akifanya vitu DRC, kocha wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Jan Borge Poulsen amemchunia kwenye kikosi chake cha wachezaji 23 cha kujiandaa na mchezo wa kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwakani nchini Afrika Kusini.
Stars itacheza na Msumbiji kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Februari 29 mwaka huu, kuwania tiketi ya AFCON mwakani.
Kikosi hicho kinachotarajiwa kuingia kambini kesho kinaundwa na makipa; Shaaban Kado wa Yanga, Juma Kaseja wa Simba na Mwadini Ali wa Azam.
Mabeki ni Stefano Mwasyika, Shadrack Nsajigwa wa Yanga, Nassor Masoud ‘Cholo’, Juma Nyoso, Juma Jabu na Kelvin Yondani wa Simba na Aggrey Morris wa Azam.
Viungo ni Jonas Gerard, Shomari Kapombe, Mwinyi Kazimoto wa Simba, Abdi Kassim na Salum Abubakar wa Azam na Shaaban Nditi wa Mtibwa Sugar, wakati washambuliaji ni Hussein Javu wa Mtibwa Sugar, John Bocco, Mrisho Ngasa wa Azam, Nizar Khalfan wa Philadelphia Union ya Marekani, Ally Badru Ally wa Canal Suez ya Misri, Uhuru Suleiman wa Simba na Nsa Job wa Villa Squad.
Samatta anatarajiwa kuiongoza tena leo Mazembe katika mchezo dhidi ya Sanga Balende nchini humo.



.png)
0 comments:
Post a Comment