• HABARI MPYA

    Monday, September 02, 2013

    WIZARA YA MICHEZO ZANZIBAR, ZFA WAPI ‘HIJA SALEH CUP’?

    IMEWEKWA SEPTEMBA 2, 2013 SAA 2:07 ASUBUHI
    KATIKA miaka ya 1950 na 1960, Zanzibar ilikuwa na wanasoka mahiri waliokuwa wakiwika hapa nchini na hata nje kupitia mashindano ya Gosssage (Sasa Challenge Cup) kwa nchi za Afrika Mashariki.
    Miongoni mwa wanasoka hao, bila shaka ni marehemu Hija Saleh ambaye kitaaluma alikuwa mwalimu wa skuli, mbali na uwezo mkubwa aliokuwa nao katika kusakata kabumbu. 
    Winga huyo machachari, alikuwa lulu si hapa Zanzibar tu akiichezea klabu ya Vikokotoni, bali pia wakongwe Young Africans SC (Yanga) ya Dar es Salaam waliutambua ufundi wake na hivyo kumtumia kila walipokuwa na mechi muhimu hasa dhidi ya watani wao wa jadi klabu ya Sunderland ambayo sasa inaitwa Simba SC.

    Yanga ilijenga utamaduni wa kumpeleka Dar es Salaam kwa ndege marehemu Hija Saleh, ili kuitumikia timu hiyo na baada ya mechi alirudi Unguja.
    Marehemu Hija Saleh pia anakumbukwa kwa kuwa muasisi wa ligi za watoto wadogo wa ngazi za junior, juvenile na central, ambazo hadi sasa zinaendelea kwa ajili ya kuibua na kukuza vipaji vya vijana katika mpira wa miguu. 
    Katika kuuenzi mchango wa mwanasoka huyo, Kamati ya Central iliamua kuanzisha mashindano maalumu kuwania Kombe la Hija Saleh (Hija Saleh Cup), ambayo yalikuwa yakishirikisha timu za vijana wadogo ambazo marehemu alisimama kidete kuziendeleza.
    Mashindano hayo yalianzishwa kwa ushirikiano mkubwa kati ya kamati hiyo na iliyokuwa Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo, wakati huo chini ya Waziri Ali Juma Shamhuna. 
    Mheshimiwa Shamhuna alivutiwa sana na fikra ya kuanzisha kwa mashindano hayo hasa kuwa kuwa naye alikuwa miongoni mwa wanafunzi wa marehemu maalim Hija Saleh katika soka.
    Katika mwaka wake wa kwanza, mashindano hayo yalipata udhamini wa Benki ya Posta Tanzania (TPB Ltd) ambayo ina tawi lake hapa Zanzibar na yakafanyika kwa ufanisi mkubwa.
    Lakini inasikitisha kwamba, matarajio ya wapenda soka wa Zanzibar kuona michuano hiyo ikendelezwa na kuimarishwa zaidi, yalipotea baada ya kuingiliwa na kidudumtu huku tamaa ya fedha ikitajwa kuwa ndiyo sumu iliyoyasambaratisha.
    Kujitokeza kwa baadhi ya watu waliopewa dhamana ya kusimamia soka hapa nchini, kulazimisha fedha za udhamini wa mashindano hayo na zile zinazopatikana kupitia viingilio zipitie mikononi kwake, ikawa sababu ya kuyaua wakati yalikwishaanza kupata umaarufu na kupendwa na kila mtu.
    Fitna hiyo ya fedha pia ikasababisha kufukuzwa kwa aliyekuwa Katibu wa Kamati ya Central Hussein Ali Ahmada, ambaye ni miongoni mwa walioyaanzisha.
    Inasikitisha kuwa sababu ya kutimuliwa kwake ni msimamo wa kutoruhusu mchezo mchafu uliolenga kuyaharibu mashindano hayo, na hapo ikawa mwisho wa kufanyika kwake.
    Kwa hali hii, ni lazima tukiri kwamba hatukumtendea haki muasisi wa ligi za watoto hapa Zanzibar marehemu Hija Saleh, kwani kuanzishwa mashindano na kuyaua baada ya mwaka mmoja tu, hakuoneshi dhamira ya kumuenzi muhusika ambaye jina lake ndilo linaloyabeba.
    Tunapoamua kuanzisha mashindano ya michezo, lazima tuwe ‘serious’ kwani haya si ya kwanza kubuniwa na kushindwa kuyaendeleza, na kwa kutaja machache, ni Kombe la Majimbo, Kombe la Ujirani Mwema, na Kombe la Urafiki ambalo lilianzishwa kwa ushirikiano na Ubalozi wa Misri hapa nchini. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: WIZARA YA MICHEZO ZANZIBAR, ZFA WAPI ‘HIJA SALEH CUP’? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top