• HABARI MPYA

    Friday, May 01, 2026

    CHOBWEDO AFUNGA LA KWANZA TRA UNITED YAICHAPA PRISONS 3-0 SOKOINE


    TIMU ya TRA United imeibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya wenyeji, Tanzania Prisons katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara jioni ya leo Uwanja wa Sokoine Jijini Mbeya.
    Mabao ya TRA United yamefungwa na winga Ramadhan Salum Chobwedo dakika ya tatu na Waganda, mshambuliaji Mganda, Joseph Akandanwaho dakika ya 63 na kiungo Khassimuh Mugoya dakika ya 75.
    Kwa ushindi huo, TRA United zamani ikijulikana kwa majina ya Tabora United na KITAYOSCE kabla ya kupanda Ligi Kuu, inafikisha pointi 30 na kurejea nafasi ya tano, wakati Tanzania Prisons inabaki na pointi zake 14 nafasi ya 15 kwenye ligi ya timu 16 baada ya timu zote kucheza mechi 20.
    Ikumbukwe mwisho wa msimu timu mbili zitashuka Daraja na mbili zitakazomaliza nafasi ya 14 na 13 zitamenyana baina yao kwa mechi mbili za nyumbani na ugenini na mshindi wa jumla atasalia Ligi Kuu.
    Timu itakayofungwa itakwenda kumenyana na timu kutoka Ligi ya Championship katika mechi nyingine mbili za mchujo nyumbani na ugenini na mshindi wa jumla ndiye atacheza Ligi Kuu msimu ujao.

    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: CHOBWEDO AFUNGA LA KWANZA TRA UNITED YAICHAPA PRISONS 3-0 SOKOINE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top