TIMU ya Fountain Gate FC imeibuka na ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Coastal Union katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara jioni ya leo Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Jijini Arusha.
Mabao ya Fountain Gate FC yamefungwa na Wanigeria, mshambuliaji Mnigeria, Chukwunonye Obasi dakika ya 15, kiungo Henry David dakika ya 33 na kiungo mzawa, Ismnail Aziz Kader dakika ya 70 wakati ya Coastal Union yamefungwa na winga Shiza Kichuya dakika ya pili na mshambuliaji Meshack Abraham Mwamita dakika ya 90’+5.
Kwa ushindi huo, Fountain Gate inafikisha pointi 22 na kusogea nafasi ya 13 ikizidiwa tu wastani wa mabao na Coastal Union iliyopo katika nafasi ya 12 kwenye ligi ya timu 16 baada ya timu hizo kucheza mechi 21 kila moja.
Ikumbukwe mwisho wa msimu timu mbili zitashuka Daraja na mbili zitakazomaliza nafasi ya 14 na 13 zitamenyana baina yao kwa mechi mbili za nyumbani na ugenini na mshindi wa jumla atasalia Ligi Kuu.
Timu itakayofungwa itakwenda kumenyana na timu kutoka Ligi ya Championship katika mechi nyingine mbili za mchujo nyumbani na ugenini na mshindi wa jumla ndiye atacheza Ligi Kuu msimu ujao.



.png)
0 comments:
Post a Comment