TIMU ya Azam FC imeibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Namungo FC katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara usiku huu Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
Bao pekee la Azam FC katika mchezo huo limefungwa na kiungo Feisal Salum Abdallah ‘Fei Toto’ dakika ya 47 kwa penalti kufuatia mshambuliaji Mkongo, Jephte Kitambala Bola kuangushwa na beki Hussein Rashid Bakari, maarufu kwa jina la utani Hussein Kazi.
Kwa ushindi huo, Azam FC inafikisha pointi 43 katika mchezo wa 21 sawa na Simba SC ambayo imecheza mechi 20 na zote zinalingana wastani wa mabao baada ya mlinganisho wa ya kufunga na kufungwa (GD) kila timu mabao 25.
Kwa upande wao Namungo FC baada ya kupoteza mchezo huo wanabaki na pointi zao 23 za mechi 21 pia nafasi ya 10 kwenye ligi ya timu 16.
Ikumbukwe mwisho wa msimu timu mbili zitashuka Daraja na mbili zitakazomaliza nafasi ya 14 na 13 zitamenyana baina yao kwa mechi mbili za nyumbani na ugenini na mshindi wa jumla atasalia Ligi Kuu.
Timu itakayofungwa itakwenda kumenyana na timu kutoka Ligi ya Championship katika mechi nyingine mbili za mchujo nyumbani na ugenini na mshindi wa jumla ndiye atacheza Ligi Kuu msimu ujao.



.png)
0 comments:
Post a Comment