MABINGWA wa Tanzania Bara, Yanga wamefanikiwa kuingia Nusu Fainali ya Kombe la Mapinduzi, michuano hiyo maalum ya kuazimisha miaka 61 ya Muungano baada ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya KVZ usiku huu Uwanja wa Gombani, Pemba.
Ilikuwa siku nzuri kwa winga Dennis David Nkane aliyetoa pasi ya bao la kwanza lililofungwa na kiungo Mburkinabe, Stephane Aziz Ki dakika ya 28, kabla ya yeye mwenyewe kufunga la pili dakika ya 86.
Yanga sasa itakutana na JKU iliyoitoa Singida Black Stars katika mchezo wa Nusu Fainali Jumanne, wakati Jumatatu itachezwa Nusu Fainali ya kwanza kati ya Azam FC na Zimamoto.
Wakati Azam FC iliitoa KMKM kwa kuichapa bao 1-0, Zimamoto pia iliitupa nje Coastal Union ya Tanga kwa kuichapa bao 1-0 pia hapo hapo Gombani.
Fainali ya michuano hiyo maalum ya kuazimisha sherehe za Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliozaa Tanzania tukufu Aprili 26 itachezwa Mei 1 hapo hapo Uwanja wa Gombani.
Mabingwa watetezi, Simba wameshindwa kushiriki michuano ya mwaka huu kwa sababu wanakabiliwa na mechi ya marudiano ya Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Stellenbosch ya Afrika Kusini kesho Jijini Durban.
Simba SC ilitwaa taji la michuano hiyo iliyoanza mwaka jana kwa ushindi wa 1-0 dhidi ya Azam FC katika Fainali Uwanja wa New Amaan Complex, bao pekee la kiungo Msenegal, Babacar Sarr, dakika ya 77.
Sarr alifunga bao hilo akimalizia mpira wa adhabu uliopigwa na beki Israel Patrick Mwenda kufuatia mshambuliaji Mcameroon, Leandre Willy Essomba Onana kuangushwa nje kidogo ya boksi.
Simba SC ilizawadiwa Sh. Milioni 50, wakati washindi wa pili, Azam FC walipata Sh. Milioni 30.
0 comments:
Post a Comment